Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

‘Mateja’ walivyo hatarini kuambukizwa VVU, ini

7fb299b5ccc80ef17cc01d64027eba82.png ‘Mateja’ walivyo hatarini kuambukizwa VVU, ini

Tue, 5 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

WATUMIAJI wa dawa za kulevya wapo hatarini kuambukizwa virusi vya ukimwi (VVU) na homa ya ini kutokana na wengi wao kujichoma sindano za dawa hizo.

Katibu Mtendaji wa asasi ya Gift of Hope, Said Bandawe alisema hayo wakati wa semina ya madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Tanga ya kuwapatia uelewa wa athari za dawa za kulevya katika jamii.

“Baada ya dawa za kulevya kuadimika watumiaji wengi wa dawa za kulevya ambao awali walikuwa wanavuta kwa kutumia sigara sasa wameingia kwenye kutumia dawa hizo kwa kuchangia sindano.”

"Hatari iliyopo ni kwamba wanapotumia sindano moja zaidi ya mtu mmoja wanajiweka kwenye hatari kubwa ya kupata maambukizi ya virusi vya Ukimwi na homa ya ini," alisema.

Bandawe alisema asasi hiyo inatoa ushauri kwa watumiaji wa dawa za kulevya kuhusu njia sahihi za kufanya na kuwaunganisha na huduma ya tiba ya methadone ili wapate tiba na kurudi katika hali zao za awali.

Alisema ili kuongeza nguvu ya jitihada wanazozichukua wameamua kutoa elimu hiyo kwa madiwani ili wasaidie kuwatambua waathirika wa dawa za kulevya katika maeneo yao waweze kuwaunganisha na tiba.

Mwakilishi wa Mamlaka ya Kupambana na Dawa za Kulevya nchini, Dk Norman Sabuni alisema licha ya serikali kusogeza huduma za methadone katika maeneo yenye athari zaidi, kuna changamoto kwenye mwitikio wa watumiaji.

“Ipo haja kwa wadau na wawakilishi wa serikali walioko katika ngazi ya jamii kuhakikisha wanashirikiana kuwabaini watumiaji wa dawa za kulevya na kuwaunganisha na tiba ili kudhibiti athari zaidi.”

"Kwa kiasi kikubwa mamlaka imefanikiwa kudhibiti uingizwaji na usafirishaji wa dawa za kulevya nchini na kinachotakiwa kwa sasa ni wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola kwa kutoa taarifa za watu wachache ambao wanaendelea kufanya biashara hii haramu," alisema Dk Sabuni.

Naibu Meya wa Jiji la Tanga, Joseph Colvas aliwataka madiwani kushirikiana na viongozi kwenye kata kuwabaini watumiaji wa dawa za kulevya na wanaojihusisha na biashara hiyo ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.

"Hili jambo sio la kulifumbia macho, sisi tunawajua wananchi wetu hivyo ili kudhibiti athari zaidi na kupoteza nguvu kazi kubwa ni lazima ifike mahali tuunge mkono jitihada zinazofanywa na serikali kutokomeza dawa za kulevya," alisema Colvas.

Chanzo: habarileo.co.tz