Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Masharti bima ya afya kwa wote

Bima Kwa Wote Masharti bima ya afya kwa wote

Sun, 25 Sep 2022 Chanzo: Mwananchi

Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote, umewasilishwa bungeni, huku ukizitaka mamlaka kadhaa zikiwamo zinazotoa usajili, vibali, hati au leseni kwa waombaji, kuzingatia kigezo cha uwepo wa uthibitisho wa uanachama katika skimu ya bima ya afya.

Muswada huo uliosomwa kwa mara ya kwanza bungeni juzi, unapendekeza hilo kufanyika kwa kuzingatia sheria zilizotungwa na Bunge na mamlaka hizo husika.

Muswada huo unazitaja mamlaka hizo kuwa ni zile zinazotoa leseni ya udereva, bima za vyombo vya moto, utambulisho wa mlipa kodi, usajili wa laini za simu, leseni ya biashara, hati ya kusafiria au viza, uandikishaji wa wanafunzi wa kidato cha tano, kidato cha sita na vyuoni na utoaji wa kitambulisho cha Taifa.

“(Mamlaka) zitahakikisha usajili au utoaji wa vibali, hati au leseni kwa waombaji, unazingatia kigezo cha uwepo wa uthibitisho wa uanachama katika skimu ya bima ya afya,” ilisema sehemu ya muswada huo ambao umekuwa ukisubiriwa kwa muda mrefu.

Pia muswada huo uliosainiwa na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, unapendekeza kwa kuzingatia utaratibu utakaoainishwa katika kanuni, mwajiri katika sekta ya umma na sekta rasmi binafsi, atapaswa kumsajili mwajiriwa katika skimu ya bima ya afya ndani ya siku 30 tangu kuanza kwa mkataba wa ajira.

Hatua hiyo ya kuwasilishwa kwa muswada huo, imekuja miezi 17 kupita tangu Aprili 22, 2021 Rais Samia Suluhu Hassan alipolihutubia Bunge la Tanzania katika hotuba yake ya kwanza tangu aapishwe Machi 19, mwaka jana ambapo aliahidi kuweka mipango na mikakati ili kila mwananchi awe na uhakika wa kutibiwa kwa kuimarisha mifuko ya bima za afya.

“Tutaimarisha mifuko ya bima ya afya ili kufikia bima ya afya kwa Watanzania wote. Kwa sasa inasikitisha Watanzania 8,224,271 ndiyo wanatumia bima ambao ni asilimia 14 tu, tutahamasisha ujenzi wa viwanda vya kutengeneza dawa, vifaa tiba na vitendanishi,” alisema Rais Samia, aliyeingia madarakani kufuatia kifo cha Rais wa awamu ya tano, hayati John Magufuli.

Muswada huo umekuja baada ya maoni ya wabunge wengi kugonga mwamba katika mikutano mbalimbali ya Bunge waliyokuwa wakikumbushia suala hilo.

Fedha zitakapopatikana

Muswada huo uliosainiwa na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, unasema kwa madhumuni ya upatikanaji wa kitita cha mafao ya msingi, kila mwajiri chini ya sekta ya umma na sekta binafsi, atawasilisha katika skimu asilimia sita ya mshahara wa mwajiriwa.

Katika asilimia hizo sita, mwajiri atachangia nusu au zaidi ya kiwango hicho na kiwango kilichosalia kitachangiwa na mwajiriwa.

Waziri kwa kushauriana na waziri mwenye dhamana ya masuala ya fedha, ataainisha viwango vya uchangiaji kwa ajili ya sekta isiyo rasmi, kama itakavyoainishwa katika kanuni, kwa kuzingatia tathmini ya uhai na uendelevu wa skimu za bima ya afya katika utoaji wa kitita cha mafao ya msingi.

Muswada huo unapendekeza kwa sekta ya umma na rasmi binafsi michango itakayotokana na mishahara inayolipwa kwa waajiriwa, hivyo kwa muktadha wa sheria hii, mshahara umetafsiriwa kwa maana sawa na inayotumika na mifuko ya pensheni..

Pia, ulipendekeza waziri, kwa kushirikiana na mamlaka zinazohusika, na kwa kupitia kanuni, kuweka utaratibu na namna ya utambuzi wa watu wasio na uwezo.

Umeongeza kuwa watu watakaotambuliwa kama watu wasio na uwezo, watakuwa na haki ya kujumuishwa chini ya skimu ya bima ya afya kwa namna itakayoainishwa kwenye kanuni.

Muswada unasema waziri mwenye dhamana ya masuala ya fedha kwa kushauriana na waziri, ataainisha vyanzo mahususi kwa ajili ya ugharamiaji wa huduma za bima ya afya kwa watu wasio na uwezo.

Adhabu kwa wakiuka sheria

Muswada unapendekeza mtu yeyote ambaye anatoa taarifa za uongo ama kushindwa kuwasilisha nyaraka zinazohitajika chini ya sheria hii pasipo kuwa na sababu za msingi, anatenda kosa na akitiwa hatiani, atawajibika.

Ulisema kwa kosa lililotendwa na mwanachama au mnufaika, kulipa faini isiyopungua Sh200,000 na isiyozidi Sh1 milioni au kutumikia kifungo kwa kipindi kisichopungua mwaka mmoja au vyote.

Endapo kosa litatendwa na skimu ya bima ya afya au kituo cha kutolea huduma za afya kilichoingia mkataba, kitatakiwa kulipa faini isiyopungua Sh5 milioni na isiyozidi Sh100 milioni.

Muswada umependekeza endapo kosa limetendwa na kampuni au taasisi chini ya sheria hiyo, kiongozi wa taasisi husika atawajibika, ikiwa atatiwa hatiani, kwa adhabu iliyoainishwa kuhusiana na kosa hilo, isipokuwa kama mkurugenzi, meneja au mbia huyo ataithibitishia mahakama kwamba kilifanywa pasipo yeye kuwa na uelewa.

Muswada pia ulipendekeza endapo kutakuwa na ukinzani baina ya masharti ya sheria hiyo na masharti ya sheria nyingine yoyote kuhusiana na masuala ya bima ya afya, masharti ya sheria hiyo yatapewa kipaumbele.

Walichokisema wadau

Akichambua muswada huo, Mwenyekiti wa Chama cha Watoa Huduma za Afya Binafsi Tanzania (Aphtha), Dk Egina Makwabe alisema Mamlaka ya Udhibiti wa Bima iliyoanzishwa chini ya Sheria ya Bima ni kitu kizuri kitakachowezesha bima ya afya kwa wote nchini kutokana na uzoefu wa kutokuwa na udhibiti hapo kabla.

“Bima zilizopo hazina mdhibiti; wao ndiyo walipaji, mahakama kila kitu tumekuwa tukilalamika sana. Sasa hivi amekuwepo mdhibiti ambapo malalamiko yote yatapelekwa pale, usuluhishi wa migogoro na kutakuwa na sheria,” alisema na kuongeza kuwa hatua hiyo itasaidia utendaji wa mfuko.

Hata hivyo, aliainisha dosari zilizopo ikiwamo mdhibiti wa mifuko hiyo kupewa haki ya kudhibiti ubora katika hospitali binafsi kitu alichokiita si kazi yake, bali inapaswa kuachwa mikononi mwa Wizara ya Afya.

Muswada huo unaeleza kuwepo na uwakilishi wa mamlaka ya bima katika bodi ya hospitali binafsi kwa lengo la kuboresha udhibiti wa hospitali hizo ambazo ni watoa huduma chini ya sheria inayopendekezwa.

Alisema pia eneo la viwango vya uchangiaji inaeleza kwamba mwajiri atatoa asilimia tatu na jumla itakuwa asilimia sita na michango ambayo inatakiwa iwasilishwe kabla ya siku 30.

“Serikalini ni rahisi lakini sekta binafsi ni ngumu. Kuna watu wanaajiriwa na matazamio ya miezi mitatu au sita itakuwaje? Kwa nini isiangaliwe baada ya kumaliza uangalizi?” alihoji.

Mhadhiri msaidizi katika usimamizi, ufuatiliaji na tathmini ya miradi ya afya kutoka Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba Muhimbili (Muhas) Pankras Luoga alisema wananchi wanatakiwa kuunga mkono suala la bima ya afya kwa wote kutokana na faida zake hasa kwa jamii isiyo na uhakika wa kipato.

Daktari bingwa wa upasuaji, Mugisha Ntiyonza Nkoronko alisema zipo tofauti nyingi mno kati ya bima inayopendekezwa na ile bima ya zamani ikiwamo wigo wa wachangiaji, unawahusisha watu wengi zaidi na sasa ni lazima kwa watu wote.

“Sheria itataka Watanzania wote kuwa na bima ya afya kwa ulazima hiyo ni pamoja na wageni wote watakaotembelea Tanzania ni lazima wawe na bima,” alisema Dk Nkoronko.

Mtaalamu na mshauri wa masuala ya afya, Dk Elisha Osati alisema: “Tunashkuru angalau muswada umeenda bungeni, tumekuwa tukipiga kelele sana tunashukuru.”

Chanzo: Mwananchi