Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Marufuku uuzaji holela vidonge vya uzazi

Ebe4345f6a4999d3775b8548e1afa2c1 Dkt.Mahundi akiwa na baadhi ya dawa zilizokamatwa

Mon, 18 Apr 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba nchini (TMDA), imewaonya wafanyabiashara wa maduka ya dawa muhimu kuachana na uuzaji holela wa vidonge vya uzazi, maarufu kama P2, kwani maelekezo ya kisheria ni dawa hizo kuuzwa kwenye maduka maalumu tu yaliyo na wataalamu wa afya.

Meneja wa TMDA Kanda ya Ziwa Magharibi, Ofisi za Geita, Dk. Edgar Mahundi, amesema kwamba Mamlaka imefanya msako kwenye maduka ya dawa muhimu mikoa ya Geita na Kagera na kubaini uuzaji holela wa P2 kwa asilimia takribani 40.

Amesema katika msako huo TMDA ulifanikiwa kupata jumla ya pakiti 87 za P2 zikiuzwa katika maduka yasiyoruhusiwa kuuza dawa hizo.

Kwa mujibu wa Meneja huyo, jumla ya maduka 81 mkoani Kagera yamekaguliwa na kukuta maduka 22 yakiuza vidonge hivyo, na maduka 65 yamekaguliwa mkoani Geita na 17 kukutwa na P2.

“Hizi tulizozikamata kwenye maduka yasiyoruhusiwa tunazirudisha vituo vya kutolea huduma. Hatua hii ni kwa mujibu wa sheria ya ada na tozo ya mwaka 2021 ya TMDA,” amesema Mahundi.

Amesema wahusika walipewa onyo kali na kupewa katazo la kuuza dawa hizo na watakaokiuka watachukuliwa hatua za sheria ikiwemo kufungiwa maduka, kunyang’anywa leseni na hata kupelekwa mahakamani.

Wakati huohuo, Mahundi amewataka wanawake kuacha matumizi holela ya vidonge hivyo, ambavyo mojawapo ya madhara yake ni kuweka usugu katika mfumo wa uzazi.

Amefafanua kwamba dawa yoyote inapotumika ndivyo isivyo inaweza kuleta madhara makubwa ya kiafya kwa mtumiaji.

“Mwenye ulazima wa kutumia dawa hizi ahakikishe anapata ushauri kutoka kwa watalaam wa afya kabla ya kumeza, na sio kununua tu na kutumia kwa jinsi anavyoamua yeye, wakati wowote,” ameonya.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live