Balozi wa Marekani Dkt. Donald Wright na Waziri wa Afya, Mheshimiwa Ummy Mwalimu, wameshiriki katika hafla ya kusherehekea miaka mitano ya mradi wa Okoa Maisha Dhibiti Malaria (OMDM) na miaka miwili ya mradi wa Impact Malaria. Pia wamezindua miradi miwili mipya ya miaka mitano (Dhibiti Malaria na Shinda Malaria) itakayogharimu dola za Kimarekani milioni 45 chini ya Mpango wa Rais wa Marekani wa Kupambana na Malaria (PMI).
Zaidi ya watu milioni 45 wako katika hatari ya kuugua malaria nchini Tanzania kutokana na hali ya nchi na topografia. Serikali ya Marekani kupitia PMI imekuwa na jukumu kubwa la kupunguza maambukizi ya malaria kutoka asilimia 18 mwaka 2015 hadi asilimia 7, kulingana na takwimu za sasa. Hata hivyo, jitihada zaidi zinahitajika ili kuutokomeza kabisa.
Tangu mwaka 2006, serikali ya Marekani imechangia zaidi ya dola za Kimarekani milioni 661 kupitia PMI kukabiliana na malaria nchini Tanzania. Uwekezaji wa Marekani katika malaria umesaidia kuimarisha mfumo wa afya wa Tanzania kwa ujumla, na kuthibitishwa kuwa muhimu katika kufuatilia matukio, usambazaji na udhibiti wa malaria. Kupunguza kuenea kwa malaria nchini Tanzania, kunawaondolea mzigo familia, na hivyo kuwawezesha watu wazima kufanya kazi na watoto kuhudhuria shule.
Miradi hii miwili mipya ya Shinda Malaria na Dhibiti Malaria iliundwa kwa ushirikiano wa karibu na Wizara za Afya za Tanzania Bara na Zanzibar na ni ishara ya mbinu ambazo serikali ya Marekani inatumia, kupitia Shirika lake la Maendeleo ya Kimataifa (USAID), kwa kushirikiana na nchi washirika kuhakikisha misaada ya Marekani ya nje ya nchi inawiana na vipaumbele vya Tanzania.
Akizungumza katika hafla hiyo, Balozi Wright alisema; “Serikali ya Marekani imejitolea kuendeleza ushirikiano na Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria pamoja na jumuiya za kiraia kama ilivyo kwa watu, mashirika na serikali ya Tanzania. Kuanzia sasa, ni lazima tuongeze dhamira yetu ya kuimarisha mifumo ya afya na juhudi za Tanzania kutokomeza ugonjwa huu hatari, unazuilika kabisa.”