Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mapendekezo kwa serikali kudhibiti ujanjaujanja tiba asilia

7c8ad67371de01fdd5c524cddbc5a602 Mapendekezo kwa serikali kudhibiti ujanjaujanja tiba asilia

Tue, 22 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

HUDUMA za tiba mbadala nchini, zilianzishwa mwanzoni mwa miaka ya 1965 na kurejelewa mwaka 1990 hadi ilipotungwa Sheria ya Tiba Asili na Tiba Mbadala ya Mwaka 2002.

Kutungwa kwa sheria hiyo, kulitoa nafasi ya kuanzishwa kwa Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala mwaka 2005. Baraza hilo limepewa mamlaka ya kuboresha huduma za tiba asili na tiba mbadala kwa upande wa Tanzania Bara.

Kutokana na umuhimu wa tiba asili na tiba mbadala katika jamii, Rais John Magufuli amewahi kuweka bayana kuwa, tiba hizi hazipaswi kupuuzwa, bali kuboreshwa ili ziwe na tija zaidi kwa jamii huku akiwashangaa baadhi ya wasomi wanaobeza tiba hizi kwa madai kuwa, zimepitwa na wakati.

Katibu Mkuu wa Shirika la Dawa Asilia na Utunzaji wa Mazingira (TRAMEPRO), Boniventura Mwalongo, anayaweka bayana mambo muhimu ambayo serikali inapaswa kuyawekea mkazo katika vituo vya tiba asili ili tiba hizo ziwe na tija zaidi kwa jamii.

Mambo haya ni pamoja na kuzingatia zaidi matakwa ya sheria katika maombi ya usajili wa muda wa mganga au mkunga wa tiba asili kwa mujibu wa wa Kifungu cha 14 (1) cha Sheria ya Tiba Asili na Tiba Mbadala namba 23 ya mwaka 2002, kifungu cha 3 cha Kanuni za Usajili.

Anasema hilo liende sambamba na maombi ya usajili wa kituo cha tiba asili kinachomilikiwa na mtu binafsi, kwa mujibu wa Kifungu cha 55 (2) cha sheria hiyo, kifungu cha 37 (1) cha Kanuni za Usajili.

Eneo lingine muhimu zaidi kuzingatia na kuwekea nguvu kubwa anasema ni katika maombi ya usajili wa kiwanda cha kutengeneza dawa za asili, kwa mujibu wa kifungu cha 55 (2) (h) cha sheria hiyo na kifungu cha 16 (1) cha kanuni za dawa.

“Kuwe na umakini mkubwa katika kushughulikia maombi ya usajili wa muda wa mganga wa tiba asili asiye Mtanzania. Hili lifanyike kwa mujibu wa kifungu cha 19 cha Sheria ya Tiba Asili na Tiba Mbadala Namba 23 ya Mwaka 2002, kifungu cha 19 cha Kanuni za Usajili,” anasema Mwalongo.

Lingine anasema ni maombi ya usajili wa kituo cha mganga wa tiba asili asiye Mtanzania kinachomilikiwa na mtu binafsi kwa mujibu wa kifungu cha 55 (2) cha sheria hiypo sambamba na kifungu cha 50 (1) cha kanuni za usajili.

Eneo lingine ni maombi ya usajili wa kituo cha mganga wa tiba mbadala kinachomilikiwa na kampuni, asasi au taasisi kwa mujibu wa kifungu cha 55 (2) cha sheria hiyo na kifungu 44 (2) cha kanuni husika.

Katibu Mkuu huyo wa TRAMEPRO, anasisitiza Serikali kutupa jicho makini katika fomu namba 13 inayohusu maombi ya usajili wa muda wa waagizaji na wauza dawa na bidhaa za kundi la pili na la tano nje ya nchi kwa mujibu wa kifungu cha 55 (2) (h) cha sheria hiyo ya tiba asili na mbadala.

“Fomu namba 15 inahusu maombi ya kibali cha kufanya utafiti wa tiba asili kwa mujibu wa kifungu cha 55 (2) cha sheria na kifungu cha 21 cha kanuni za dawa.

Fomu namba 16 ni maombi ya usajili wa kundi la pili la dawa, zana, vifaa na mashine kwa mujibu wa kifungu cha 55 (2) (i) cha sheria na kifungu cha 11 (2) cha kanuni za dawa.

“Lingine muhimu ni maombi ya usajili wa kundi la tano la dawa, zana, vifaa na mashine kwa mujibu wa kifungu cha 55 (2) (i) na kifungu cha 11 (2) cha Kanuni za Dawa.

Kwa kuzingatia maeneo hayo, Mwalongo anatoa ushauri kwa Serikali kuangalia uwezekano wa kuwapo kongamano la kitaifa kuhusu uvunaji wa miti dawa endelevu ili uwe mjadala mpana kwa serikali, vyuo vikuu na wadau.

“Pendekezo lingine kwa serikali ni vyuo na taasisi zisizo za kiserikali, kuandaa mitaala ya mafunzo na kuwashirikisha wataalamu wa tiba asili,” anasema Mwalongo.

Kwa mujibu wa Mwalongo, ushauri mwingine kwa serikali ni kuweka mkazo na kupiga marufuku suala la imani za kishirikina na upigaji ramli kuhusishwa na tiba asili.

Katibu Mkuu huyo wa TRAMEPRO anasema: “Ushauri mwingine kwa serikali ni kwamba, imani za kishirikina na upigaji ramli visihusishwe na tiba asili na yeyote anayebainika kushiriki, achukuliwe hatua kali za kisheria…”

Anaongeza: “Pia, kusiwepo matangazo katika vyombo vya habari yasiyo na kibali cha Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala kwa ushirikiano na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na pia, wauzaji katika maduka au stoo za dawa asili, wapate mafunzo ya kuendesha huduma hizo.”

Kwa mujibu wa shirika hilo, ni vyema huduma za tiba asili na tiba mbadala zitolewe kwa kufuata mwongozo na ushauri makini na kutotoa ruhusa kwa wasio na mafunzo ya tiba asili na tiba mbadala kutoa huduma hizo.

“Tunashauri pia waganga wote wa tiba asili na tiba mbadala kuwa tayari kwa ukaguzi kutoka ofisi ya mganga mkuu wa wilaya husika na vitambuliwe vituo maalumu vinavyotoa huduma za mama na mtoto na magonjwa ya akili.

Mwalongo pia anawakumbusha wanachama na wadau wote wa tiba asili nchini katazo la Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyama Pori Tanzania (Tawa) kwa wanaotumia nyara katika tiba kutokana na kurithi kwa wahenga.

“Katika Siku ya Wanyamapori Machi 3, 2019, Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyama pori Tanzania, ilitoa taarifa kwa umma ikizuia kuvaa, kununua au kumiliki nyara za serikali kinyume cha Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori Namba 5 ya Mwaka 2009 bila kibali cha mkurugenzi wa wanyamapori na kutoa mwito aliye navyo kuwasiliana na Tawa au TRAMEPRO kwa maelekezo,” anasema Mwalongo.

Chanzo: habarileo.co.tz