Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mapato ya NMB Marathon kutibu wagonjwa wa Fistula CCBRT

Nmb Kubwa 5454 Uzinduzi wa NMB marathon

Tue, 17 Aug 2021 Chanzo: ippmedia.com

Benki ya NMB imesaini makubaliano ya ushirikiano na hospitali ya CCBRT, yanayolenga kukusanya kiasi cha sh.Billion 1 za matibabu ya Fistula kwa kina mama wasio na uwezo, kupitia mbio za hisani za NMB Marathon zitakazofanyika kwa mara ya kwanza September 18,2021 jijini Dar es salaam.

Kupitia mbio hizo ambazo mwaka huu zitafanyika chini ya kaulimbiu ya: 'Mwendo wa Upendo,' Benki ya NMB na CCBRT wanatarajia kukusanya zaidi ya Sh. Milioni 250 kila mwaka kwa miaka minne ambazo zitasaidia matibabu ya wagonjwa wa fistula, miongoni mwa mamia ya kina mama wanaoteseka kwa maradhi hayo.

Akizungumza wakati wa utilianaji saini wa makubaliano hayo, Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna, alibainisha kuwa, Fistula ni maradhi yanayotesa kina mama wengi nchini, na akawataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kujisajili kushiriki mbio hizo, ili kufanikisha lengo la kukusanya fedha ya matibabu ya wagonjwa hao.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa CCBRT, Brenda Msangi, amesema taasisi yake inajisikia faraja kubwa kufanikisha utilianaji saini wa makubaliano hayo, sambamba na uzinduzi wa NMB Marathon 2021, huku akieleza kuwa mashindano hayo yana maana kubwa kwa maelfu ya kina mama wa Kitanzania.

NMB Marathon zitakuwa na sehemu tatu ambazo ni mbio za kilomita 21 (nusu marathon), kilomita 10 na kilomita 5, ambako washindi wa kwanza hadi wa 10 watapata medali na fedha taslimu.

Kwa mujibu wa Mratibu wa NMB Marathon 2021, David Marealle, ada ya kujisajili kushiriki mbio hizo ni Sh. 30,000 kwa kilomita 21 na Sh. 20,000 kwa mbio za kilomita 10 na kilomita 5.

Washindi wa mbio za kilomita 21 wanaume na wanawake watajinyakulia Medali ya Dhahabu na fedha taslimu Sh. 1,400,000, huku washindi wa pili wakitarajiwa kutwaa Medali za Fedha na Sh. 1,100,000, wakati washindi wa tatu wakitengewa Sh. 700,000 na Medali za Shaba.

Huku kwa mbio za kilomita 10, 700,000 na medali ya dhahabu, 500,000 na medali ya fedha pamoja na 300,000 na medali ya Shaba kwa mshindi wa kwanza, pili na tatu kwa wanaume na wanawake.

Katika mbio za kilomita 5, washindi upande wa wanawake na wanaume watajipoza na Medali za dhahabu na Sh. 250,000, washindi wa pili medali za fedha na Sh. 150,000, huku washindi wa tatu wakiambulia medali za shaba na Sh. 100,000 taslimu.

Tayari kampuni za Bima za UAP na SANLAM wameshachangia jumla ya shilingi milioni 100 (sawa na Sh. Mil. 50 kila moja).

Chanzo: ippmedia.com