Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maofisa afya wakumbushwa maadili

B92e941e37b5727375617a0ed1530fbb Maofisa afya wakumbushwa maadili

Fri, 18 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MAOFISA afya ngazi zote wametakiwa kufanya kazi zao kwa weledi na kufuata maadili wakati wanapotimiza majukumu yao katika jamii.

Kauli hiyo imetolewa jana na Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Idara kuu ya Afya, Profesa Mabula Mchembe wakati akifungua Mkutano wa Maofisa Afya mazingira wenye kaulimbiu ya "Zingatia Mahitaji ya Jinsia kwa Usafi wa Mazingira Endelevu" uliofanyika jijini Dodoma.

Aliwataka kusimamia maadili na kuhakikisha kuwa kunakuwa na ufanisi kwenye kazi wanazozifanya.

“Usitende kitu kwa kufikiria kwamba unamfanyia fulani, natambua changamoto zipo katika baadhi ya sehemu, lakini tunahitaji kutimiza wajibu wetu kwa maadili na uwaminifu wa hali ya juu," alisema.

Pia aliwataka maofisa afya mazingira kusimamia usafi katika maeneo ya huduma za vyoo katika jamii, hususani katika ofisi na vituo vya daladala ambavyo hudumia jamii kwa kiasi kikubwa ili kuikinga jamii dhidi ya magonjwa ya milipuko.

Aliwaagiza maofisa afya mazingira nchini kusimamia usafi na ubora wa vyakula katika maeneo yote yanayotoa huduma za vyakula, yakiwemo maeneo ya migahawa na hoteli ili kuikinga jamii na magonjwa ya tumbo na kuhara.

Alitoa wito kwa maofisa afya mazingira kujiepusha na vitendo vya rushwa wakati wa wakitimiza majukumu yao na kuhakikisha usafi wa mazingira unaendelea kufuatwa katika ngazi zote za Jamii.

"Tuachane na rushwa, inawezekana baadhi ya sehemu unafika pale, unapewa 10,000 au unapewa bia mbili au tatu unaondoka zako, kitu ambacho hakina maana, sasa kama wewe ni Mtaalamu wa afya simama kwenye maadili yako," alisema.

Hata hivyo, aliwaagiza maofisa afya mazingira nchini, kusimamia udhibiti wa takataka zinazotokana na utoaji wa huduma za afya ili kuendelea kuikinga jamii dhidi ya maambukizi yatokanayo na taka hizo.

Kwa upande wake, Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali, ambaye pia ni Mkurugenzi wa huduma za Kinga Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Leonard Subi aliwaagiza waganga wakuu wa mikoa kutoa elimu mara kwa mara kwa watendaji wao juu ya maadili badala ya kusubiri kuchukua hatua baada ya kosa kujitokeza.

Chanzo: habarileo.co.tz