Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maneno chanya yanakuza tabia njema

13142 Cristian+Bwaya TanzaniaWeb

Tue, 21 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

“Mbona bado umelala?” anauliza Mzee Mapunda. Kusikia hivyo, Erick anakurupuka kitandani. Huku akiwa bado hajielewi vizuri shauri ya usingizi, Erick anasikia sauti kali kutoka kwa baba yake, “Bado unafanya nini we mtoto? Harakisha uende shule.”

“Ona hata viatu hujasafisha. Una matatizo gani wewe mtoto?” Kwa unyonge Erick anashika viatu akisafishe.

Ile haraka ya kufanya kile anachotaka baba yake, anajikuta amesahau kupiga mswaki. Mzee Mapunda anamstua kwa kumzaba kibao, “Mswaki apige nani mbona unakuwa mtu wa ajabu hivyo. “Fanya haraka gari linakuacha.”

Erick anajivutavuta kuondoka nyumbani akiwa na huzuni. Moyoni mwake anawaza kosa lake ni lipi?

Baadaye jioni, Erick anaporudi nyumbani mnyororo wa maneno hasi unaendelea. “Mbona hufanyi kazi za nyumbani? Muone alivyo mvivu.” Erick anashika madaftari kusoma. Mapunda anamkemea; “Kwa nini umekasirika, we vipi? Unajua ninalipa ada kiasi gani?” Erick anaondoka sebuleni. “Unaondoka, muone kwanza.”

Huu ni mfano wa maisha yetu na wanetu nyumbani. Muda mwingi tunawaambia maneno yanayotuma ujumbe hasi na maisha yao.

Tunawalaumu. Tunawaonyesha upungufu wao. Tunawakemea. Matokeo yake wanaanza kuwa na wasiwasi na uwezo wao. Wanaanza kuamini wana upungufu fulani.

Tunayafanya hayo wakati kwa upande mwingine, tunajiuliza inakuwaje unaweza kumwadhibu mtoto, ukamwelekeza nini cha kufanya na bado asifanye? Inakuwaje mtoto anakuwa na nidhamu mbele ya mzazi lakini akiwa mbali na mzazi anakuwa na tabia nyingine? Kwa nini mtoto asiye na nidhamu kwa mzazi fulani anaweza kuwa mnyenyekevu kwa mzazi mwingine? Tatizo ni nini?

Ukweli ni kwamba, pamoja na sababu nyingine, maneno na tabia zetu kama wazazi zina mchango mkubwa katika kujenga tabia za watoto.

Kukosa adabu, kwa mfano, hakutokei kwa bahati mbaya. Mtoto kwa kawaida hazaliwi na msukumo wa kushindana wala kumkosea adabu mzazi. Badala yake, huzaliwa na fahari ya kumpendeza na kushirikiana na mzazi.

Sasa tujiulize kwa nini hufika mahali mtoto akaanza kujisikia fahari kushindana na mzazi? Tukitumia mfano wa Mapunda, inawezekana akawa na nia njema na mwanawe.

Lakini asichokijua Mapunda ni kwamba maneno yake kwa Erick yanaweza kuwa kinyume na matarajio yake.

Ule ukaribu wa kawaida kati yake na Erick utaendelea kuzorota kwa sababu kila anachomwambia Erick kinamfanya ajione ana upungufu. Hakuna binadamu anayependa kujiona ana upungufu.

Inawezekana Mapunda alikuwa karibu na Erick akiwa na umri mdogo. Lakini kadri Erick alivyoendelea kukua kimwili, Mapunda akaanza kukasirishwa na baadhi ya tabia anazoonyesha Erick.

Makosa na kutofanya kile anachoambiwa kukaanza kumfanya Mapunda awe mbali na mwanawe na hivyo akaanza kupunguza jitihada za kushirikiana naye.

Tunafahamu kwa mfano, wazazi wengi tumeacha kucheza na watoto wetu. Walipokuwa wadogo tuliwarusharusha kwa furaha, lakini walipokuwa wakubwa tukaanza kusita kufanya hivyo.

Badala ya kuwa karibu na watoto wetu, tunajenga mazoea ya kuwashambulia na kuonyesha upungufu wao kama anavyofanya Mapunda.

Mazoea kama haya, yanamjengea mtoto uhitaji mkubwa wa ndani kwa ndani. Mtoto anakuwa na shauku ya ukaribu usiopatikana.

Ukaribu unapokosekana huchochea jitihada za kisaikolojia za mtoto kuziba pengo analojisikia ndani yake. Moja wapo ya jitihada hizi ni kufanya vituko ambavyo mzazi anaweza kuvitafsiri kama kukosa nidhamu.

Ni vizuri kutambua kuwa mtoto anapofanya hivyo, nia yake hasa si kumuudhi mzazi. Hapana. Hawezi kutaka kumuudhi mzazi kwa sababu, kwa asili, ana shauku ya kushirikiana naye.

Kwa upande mwingine, kuna tatizo la sisi wazazi kupuuza hisia za mtoto kwa sababu tu tunaamini hisia hizo hazina msingi.

Hata hivyo, tunapofumba macho tusielewe hisia hizo, mtoto anajenga imani kuwa hana umuhimu kwa mzazi wake.

Unaweza kufanya kitu kidogo pasipo nia mbaya. Labda umeahidi zawadi na hujatekeleza. Labda umemkejeli mbele ya wenzake. Labda umemwambia mtoto mwingine maneno mazuri na hujamwambia yeye.

Kwako uliye mtu mzima, huoni tatizo. Kwa kujua hukuwa na nia mbaya, unaweza ukaamua kupuuza vile anavyojisikia mtoto kwa sababu unajua hayo anayoyafikiri hayana ukweli wowote.

Jambo la kuzingatia ni kuwa hisia hata kama zimejengwa kwenye dhana potofu zinaathiri kwa kiasi kikubwa mtazamo wa mtoto.

Mtazamo potofu huongoza maamuzi potofu anayoyafanya mtoto. Mathalani, mtoto anayeamini hapendwi hata kama kiukweli anapendwa atakuwa tayari kushindana na mzazi.

Kushindana na mtoto mwenye mtazamo potofu kunaweza kuchangia kukuza tabia mbovu.

Kuna umuhimu basi wa mzazi kuvaa viatu vya mtoto na kuelewa hisia zake, anafikiri nini, anaamua nini na kwa sababu gani.

Hata hivyo, katika kufanya hivyo, ni muhimu kuchukua tahadhari tatu kubwa. Kuepuka kumdekeza mno mtoto, kumdhibiti na kumwadhibu kupita kiasi.

Kudekeza ni kumlinda mtoto kupita kiasi kwa lengo la kumfanya ajione mtu mwenye umaalum usio wa kawaida. Wazazi wenye mtoto mmoja, mathalani, wanakuwa na uwezekano mkubwa wa kumchukulia mtoto kwa umaalum. Mtoto anayedekezwa hufikia kujiona bora kuliko watu wengine.

Unapomdekeza mwanao kumbuka kuwa unatengeneza hatari ya kumfanya aamini usalama wake unategemea kiasi gani anajidekeza kwako.

Pia, anaweza kujiona mtawala anayeweza kuwaendesha wengine atakavyo yeye.

Kwa upande mwingine, mtoto huyu ana uwezekano mkubwa wa kushindwa kufanya vitu vingi bila msaada wa mtu mwingine.

Huu ni upungufu unaoweza kufanya maisha yake yawe magumu pindi atakapoondoka nyumbani.

Ili kuepuka kumdekeza mtoto, punguza kumwonea huruma. Mpe nafasi ya kukabiliana na magumu na hata ikibidi kuumia kidogo kwa lengo la kujifunza maisha halisi.

Usimnyime mwanao maumivu, lakini pia usimwumize bila sababu.

Ninachojaribu kukisema hapa ni kwamba wazazi tunahitaji kuelewa kuwa maneno yetu na matendo yetu yana nguvu kubwa. Badala ya kuwalalamikia muda wote, tujenge tabia ya kusema maneno yanayowajenga kisaikolojia.

Chanzo: mwananchi.co.tz