Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mambo matatu chanzo ndoa nyingi kuvunjika

51090 Pic+ndoa

Mon, 8 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Kama ndoa yako imedumu kwa miaka kadhaa mkiwa na furaha, ni jambo jema.

Hali imekuwa tofauti, maombi ya talaka kwa wanandoa yanazidi kuongezeka katika maeneo mbalimbali nchini.

Baadhi ya sababu za hali hiyo imeelezwa kuwa ni pamoja na ukosefu wa uaminifu baina ya wanandoa, ukatili na hali ngumu ya maisha.

Mbali ya kuongezeka kwa ndoa zilizo katika foleni ya kuvunjwa, baadhi ya wanandoa ‘wanakufa na tai shingoni’ ndani ya nyumba zao, hakuna amani miongoni mwao.

“Unaona watu mbele ya jamii ni mume na mke, lakini nyumbani moto unawaka. Wanaishi nyumba moja lakini vyumba tofauti ili kulea watoto tu,” alisema mtaalamu wa saikolojia aliyeomba jina lake lisitajwe.

Alisema ndoa zimekuwa na changamoto kubwa katika zama za utandawazi ambazo zimeanza kubadili utamaduni wa Watanzania.

Meneja Uhusiano na Masoko wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita), Josephat Kimaro alisema kwa mwaka 2018, walisajili talaka 3,814 nchi nzima, lakini akasema idadi inaweza kuwa kubwa.

“Unajua utaratibu ni kwamba wakishamalizana huko mahakamani na talaka ikatolewa sheria inataka huo uamuzi uletwe Rita ili usajiliwe na hapo ndipo inahesabika ni talaka,” alisema Kimaro. “Tatizo ni kwamba talaka zikishatolewa huko watu wanaona tayari ndio mambo yameisha, lakini kisheria ni lazima iletwe hapa tuisajili na kufuta cheti cha ndoa.”

Kimaro alisema Rita inafanya mazungumzo na Mahakama kwa kutumia kwa pamoja mfumo wa kielektroniki ‘e-system’ ili talaka inapotoka waweze kuiona.

“Kwa vile wengi wakishapata ile hukumu ya talaka hawaji tena Rita inawezekana hata hii idadi ya talaka 3,814 tulizozisajili mwaka 2018 zikawa ni ndogo. Mfano Kilimanjaro tumesajili talaka tano tu mwaka 2018,” alisema.

Kuhusu Mkoa wa Kilimanjaro, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, Frank Mahimbali alisema mwaka 2018 yalifunguliwa mashauri 104 ya talaka, huku talaka zilizotolewa zikiwa 83.

“Kwa mahakama za mwanzo, kwa mwaka 2018, zilifunguliwa kesi 93 za talaka na zilizotolewa zilikuwa 77. Katika mahakama za wilaya, yalifunguliwa mashauri kumi na moja,” alisema Mahimbali.

Mambo matatu

Ofisa Ustawi wa Jamii, Manispaa ya Moshi, Duncan Mgati alisema maombi ya talaka yameongezeka. Kuthibitisha hilo alisema mwaka 2016 kulikuwa na maombi matatu tu ya talaka yaliyowasilishwa katika ofisi yake lakini mwaka 2017 yaliongezeka na kufikia 11 huku mwaka jana yakifikia 27.

“Maombi ya kudai talaka, yameendelea kuongezeka ikilinganishwa na miaka ya nyuma na hili linasababishwa na sababu mbalimbali, lakini waathirika ni watoto,” alisema Mgati.

Alisema watoto wengi wamekuwa wakiumia na kuathirika kisaikolojia na kiakili kwa kiasi kikubwa baada ya talaka kutolewa kutokana na baadhi ya wazazi kupunguza malezi kwao.

“Unakuta watoto wanasoma shule nzuri za mifumo ya Kiingereza lakini baada ya talaka, baba anagoma kutoa ada. Hii husababisha watoto kurudishwa kwenye shule za kawaida.”

Mgeti alisema hali hiyo huwarudisha nyuma watoto kitaaluma na kusema wanapoathirika kiakili na kisaikolojia katika umri mdogo ni vigumu kufanya vizuri katika masomo yao.

Alizitaja baadhi ya sababu za takala kuwa ni ukosefu wa uaminifu baina ya wanandoa, ukatili na hali ngumu maisha.

“Asilimia kubwa ya wanaoleta maombi ya talaka ni wanawake na miongoni mwa sababu ni kupungua kwa uaminifu katika ndoa, lakini pia lipo suala la ugumu wa maisha” alisema, “unakuta wakati mwanamke anaolewa, mwanaume alikuwa na hali nzuri kifedha sasa inavyobadilika, mwanamke anakimbilia kuomba talaka kwa sababu maisha aliyoyatarajia yamebadilika.

“Lakini pia lipo suala la ukatili. Wapo wanaume ambao wamekuwa wakiwafanyia wake zao vitendo vya kikatili na vinaposhindwa kuvumilika ndipo wanakuja kuomba talaka.”

Kauli ya viongozi wa dini

Askofu mstaafu wa Kanisa la Assemblies Of God (TAG), Glorious Shoo alisema pamoja na tatizo la talaka, lipo pia la watu kuachana au kuishi pamoja huku wakiwa hawana ushirikiano.

“Kuna watu ambao wameachana bila kupeana talaka, hili nalo ni baya sana. Kuna watu wengine wanaishi pamoja lakini ukweli ni kwamba wameachana kwa maana kwamba hawana ushirikiano kwenye lolote wala chochote. Hii ni shida nyingine iliyoko kwenye ndoa kwa sasa.

Alisema sababu nyingine ya ndoa kuvunjika ni utandawazi na kukosekana mafundisho sahihi kabla ya wahusika kuoana.

“Vitu ambavyo watu wanalisha macho yao leo vinaleta shida kubwa kwenye ndoa. Watu wengi leo wanatamani kuishi maisha ya filamu siyo uhalisia, wanakuwa na matarajio ya juu,” alisema na kuongeza, “wanatarajia wakutane na raha tu, hawajui kuna wakati wanaweza kununiana au kupishana kauli, hivyo wakikutana na hali hiyo wanashangaa na ndipo matatizo huanza.”

Katibu wa Bakwata, Mkoa wa Kilimanjaro, Awadh Lema pia alitaja kuporomoka kwa maadili na utandawazi kuwa ni vyanzo vikubwa vya wanandoa kutalikiana.

“Hizi zinazoitwa tamthilia zimechangia ndoa nyingi kuvunjika. Wapo vijana wanaoana wakiwa tayari wamezoeana na kuchokana jambo ambalo ni hatari katika ndoa.”

Lema alisema sasa ndoa zimekuwa kama biashara kwa wapendanao tofauti na zamani huku akisema siku hizi wengi huchagua viongozi wa kuwafungisha ndoa tofauti na zamani.

Mkuu wa KKKT, Dk Fredrick Shoo hakuwa na mtazamo tofauti, alisema chanzo cha talaka ni kudhoofika kwa misingi ya familia na kutozingatia ahadi walizopeana, “siku hizi watu wengi hawazipi umuhimu zile ahadi wanazopeana wakati wa kuoana, wanazichukulia kama jambo jepesi na kuzingatia sherehe na mavazi.”

Askofu Shoo alisema ipo haja kwa viongozi wa dini, familia na jamii kulitazama suala hilo kwa jicho pana ili uwepo muda wa kutosha wa kuwashauri wale wanaotaka kuingia kwenye ndoa.



Chanzo: mwananchi.co.tz