Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mambo makuu matano yaliyogunduliwa tangu kuzuka kwa janga la Corona

Mambo Matano Corona Mambo makuu matano yaliyogunduliwa tangu kuzuka kwa janga la Corona

Thu, 6 Jan 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Imepita miaka miwili tangu virusi vipya vya corona kugunduliwa baada ya mlipuko wa ugonjwa huo nchini China.

Nchi hiyo ilitangaza ugunduzi wa Sars-Cov-2, ambayo husababisha covid-19, mnamo Desemba 31, 2019, na tangu wakati huo, ulimwengu umebadilika kwa kasi kubwa. Janga hili limebadilisha kuanzia jinsi tunavyofanya kazi hadi matibabu yanayopatikana kwetu.

1. Chanjo za mRNA hufanya kazi na zinaweza kutengenezwa kwa haraka

Mara tu covid-19 ilipofikia kiwango cha kuitwa janga, mbio zilianza kati ya watafiti kutengeneza chanjo ambayo inaweza kulinda watu.

Baadhi ya makampuni ya dawa yaliamua kutumia aina mpya ya teknolojia, ambayo haijawai kutumika katika chanjo iliyoidhinishwa kwa matumizi ya binadamu - mRNA.

Kwa kutumia mRNA, sio tu kwamba Pfizer/BioNTech (na baadaye Moderna) iliweza kutengeneza chanjo ya covid-19 haraka kuliko kampuni nyingine yoyote, pia ilifungua mlango kwa matibabu mengi mapya kwa kutumia teknolojia kama hiyo.

Katika chanjo za virusi vya corona, mRNA huelekeza seli zetu kuunda sehemu ndogo ya virusi vya covid. Kisha mfumo wa kinga ya mwili hujifunza kutambua virusi na huwa tayari kushambulia ikiwa mwili wako umeambukizwa.

Lakini mRNA ina uwezo wa kutumika kwa njia nyingine nyingi. Mbali na kutumika kutengeneza chanjo mpya za magonjwa kama vile VVU, mafua na Zika, inaweza kutumika kufundisha mfumo wa kinga ya mwili kushambulia seli za saratani, kuunda protini ambazo hazipo kwenye seli za watu walio na ugonjwa wa cystic fibrosis, au kufundisha mfumo wa ulinzi wa mwili kwa watu wenye sclerosis nyingi kuacha kushambulia mfumo wa neva.

Utafiti kuhusu matibabu ya kutumia mRNA umekuwa ukiendelea kwa miongo kadhaa, lakini chanjo za covid-19 ndipo teknolojia hiyo imethibitishwa kufanya kazi. Mafanikio haya yanaweza kuchochea utafiti na uwezo wa kubadilisha maisha ya mamilioni ya watu.

2. Covid-19 huenea hewani kwa urahisi zaidi kuliko tulivyofikiria mwanzoni

Takriban miezi minne baada ya janga hilo kuanza, Shirika la Afya Ulimwenguni halikushauri watu kuvaa barakoa. "Hatupendekezi kuvaa barakoa isipokuwa kama wewe ni mgonjwa," Maria Van Kerkhove, mkuu wa kiufundi wa mapambano ya Covid-19 katika shirika hilo.

Lakini ushahidi wa kisayansi ambao umeibuka tangu wakati huo umebadilisha maoni hayo. Leo hii, kama wakati mwingine wa janga hilo, WHO inasema kwamba watu wanapaswa " kuichukulia kama kawaida uvaaji barokoa wakiwa karibu na watu wengine".

Watafiti wamegundua kuwa virusi vya covid-19 huenezwa sio tu na matone makubwa ya mate au kamasi ambayo iko hewani kwa muda mfupi baada ya mtu kukohoa au kupiga chafya.

Virusi hivyo pia vinaweza kuenea kupitia erosoli - chembe ndogo zaidi ambazo zinaweza kukaa hewani kwa muda mrefu zaidi.

Sasa tunajua kwamba maambukizi ya Covid-19 ni ya hewa. Usambazaji wa Sars-CoV-2 baada ya kugusa nyuso sasa unachukuliwa kuwa mdogo.

Virusi hivyo hutolewa na watu wasio na barakoa wakati wa kuzungumza, kuimba au kupumua tu na kubaki hewani ikiwa chumba hakina hewa ya kutosha.

Kuosha mikono na kusafisha nyuso bado ni tabia nzuri, lakini sasa kuna mkazo zaidi juu ya kuvaa barakoa na uingizaji hewa.

3. Kazi za kufanyia nyumbani zitadumu kwa muda mrefu

Mamilioni ya watu ulimwenguni kote walianza kufanya kazi kutoka nyumbani badala ya kwenda ofisini na sehemu zingine za kazi wakati wa janga hilo.

Janga hili lilionyesha kuwa aina hii ya kazi haipunguzi tija na kufanya kampuni nyingi kuachana na upinzani wao wa kuitumia

Twitter ilitangaza mnamo Mei 2020 kwamba wafanyikazi wake wanaweza kufanya kazi wakiwa nyumbani kwa muda wote hata baada ya janga kumalizika, mradi tu jukumu lao linawaruhusu kufanya hivyo.

"Miezi michache iliyopita imethibitisha kuwa tunaweza kufanya kazi hii," kampuni hiyo ilisema.

Facebook ilitoa tangazo kama hilo mapema mwaka huu, lakini sio tu kampuni za teknolojia zilizo na nia kubadilisha.

Utafiti wa makampuni 1,200 uliofanywa na shirika la Enterprise Technology Research ulionyesha kuwa asilimia ya wafanyakazi duniani kote wanaofanya kazi za kudumu wakiwa nyumbani inatarajiwa kuongezeka maradufu ifikapo 2021.

4. Janga hili limewakumba zaidi watu walio katika mazingira hatarishi ya kijamii

Janga la covid-19 lilitukumbusha kuwa mzozo unaweza kuzidisha usawa mkubwa wa kijamii ambao tayari upo ulimwenguni.

Nchini Uingereza, utafiti uliofanywa uligundua kuwa katika sehemu maskini zaidi ya nchi asilimia 11.4 ya watu waliambukizwa covid, wakati katika maeneo watu wana kipato kizuri kiwango kilikuwa cha chini yaani asilimia 7.8.

Utafiti huo pia uligundua kuwa watu kutoka jamii za wachache waliathiriwa zaidi, jambo ambalo pia lilitokea nchini Marekani.

Huko New York, data za 2020 zilionyesha kuwa wa Hispanic na wale weusi walikumbwa na asilimia 34 na 2 ya vifo vya covid, mtawaliwa, ingawa wanachukua asilimia 29 na 2 ya idadi ya watu.

Katika nchi nyingi hakuna data sahihi juu ya athari za covid, lakini kimataifa moja ya tofauti kubwa ni katika chanjo. Kwenye nchi za kipato cha juu na cha kati, takriban asilimia 70 ya watu wamechanjwa kikamilifu, kulingana na data kutoka shirika la Our World in Data. Hii inashuka hadi asilimia 4 tu katika nchi zenye kipato cha chini. Hata katika nchi za kipato cha kati, kiwango bado ni asilimia 32 tu.

5. Hatuna uhakika jinsi, au kama janga la covid-19 litaisha

Katika magonjwa mengi, kama vile ndui, inawezekana kufikia kinga ya watu kupitia chanjo kwa watu wengi - ambayo ni idadi kubwa ya watu waliochanjwa hivi kwamba virusi haviwezi kusambaa.

Kwa magonjwa mengine, kama vile mafua, hii ni vigumu zaidi kufikia kwa sababu ya mabadiliko ya mara kwa mara ya virusi au kupungua kwa mfumo wa kinga kwa muda.

Kwa upande wa Covid-19, inatuonyesha kuwa tunaweza kuwa tunakabiliwa na kisa cha pili. Kupungua kwa mwitikio wa mfumo wa kinga baada ya muda ni sababu hata nchi nyingi (ikiwa ni pamoja na Brazili) zinatekeleza programu za kuongeza chanjo.

Kulingana na Shabir A Madhi, profesa katika Chuo Kikuu cha Witwatersrand nchini Afrika Kusini, mwitikio wa kinga baada ya kuambukizwa au chanjo dhidi ya covid-19 hudumu takriban miezi sita hadi tisa.

Ingawa chanjo ni nzuri katika kulinda dhidi ya athari mbaya zaidi za covid, hata zile bora zaidi hazionekani kuwazuia watu kusambaza virusi kwa wengine.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live