Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mama wa Kimasai ajifungua mapacha kwa upandikizaji

Mapacha 4.jpeg Ni miongoni mwa wanawake 9 waliopandikizwa mimba

Tue, 5 Apr 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mama Martha Sangwa kutoka wilaya ya Simanjiro, Mkoani Manyara anakuwa mwanamke wa kwanza wa kimasai, kujifungua watoto, tena mapacha, kupitia njia ya upandikizaji mimba.

Martha (36)ambaye amejifungua watoto wawili katika hospitali ya Avinta Care ya jijini Arusha, anasema amekuwa akihangaika kutafuta mtoto kwa zaidi ya miaka kumi.

Mwanamke huyo aliwataka wanawake kujitokeza kwa wingi kuchangamkia fursa hiyo kwa kuwa haihusiani na imani za kishirikina bali ni huduma inayotolewa na wataalamu waliobobea katika masuala ya uzazi

Yeye ni miongoni mwa wanawake tisa wanaopata huduma hiyo ya kupandikiziwa watoto katika hospitali hiyo iliyopo mtaa wa Jacaranda, eneo la Uzunguni mjini Arusha.

“Kati ya wanawake hao tisa, tayari watano wamefanikiwa kupata watoto, baadhi yao wakijifungua mapacha hivyo kufanya idadi ya watoto wote waliozaliwa kwa njia hii kuwa nane,” alisema Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Akina Mama, Nicholaus Mazuguni.

Kwa mujibu wa Daktari Mazuguni, Kliniki ya Avinta Care hutoa huduma hiyo kwa kushirikiana na hospitali ya taifa ya Muhimbili, Dar-es-salaam

Aidha alipongeza serikali ya awamu ya siti chini ya Rais Mama Samia Suluhu kwa jitiada kubwa ya kuhakikisha afya nzuri ya akina mama na hasa afya ya uzazi

"Katika hotuba yake mwaka jana mwezi wa 12 katika sherehe za Uhuru,Mh Rais alisema Serikali imejipanga kuhakikisha kwamba siku za usoni huduma ya tiba ya upandikizaji mimba katika taasisi za serikali hasa Muhimbili inakuwepo"alisema Dkt Mazuguni

Aliongeza kuwa huduma hii inafanywa na watanzania wazawa lakini mwanzoni iliaminika kuwa wanaoweza kutoa tiba hii ni madaktari bigwa kutoka India,Afrika kusini na Narobi tena kwa gharama kubwa

Naye Mganga Mkuu wa mkoa, Dk Sylvia Mamkwe, aliyemuwakilisha Mkuu wa Mkoa, katika uzinduzi wa huduma hiyo maalum ya uzazi, amesema katika utoaji wa huduma bora za afya, serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi.

Dk Mamkwe amewashauri watanzania kutoogopa kutumia njia hizi mbadala za tiba katika uzazi, muhimu tu ni kupima na kuhakikisha afya zao.

“Lakini pia katika masuala ya matatizo ya uzazi mara nyingi wanawake ndio hulaumiwa, kitu ambacho sio sahihi. Wazazi wote wawili wanatakiwa kupima afya zao,” alisema Dokta Mamkwe.

Mganga huyo wa mkoa amebainisha pia kwamba, wakati mwingine kushindwa kupata watoto hutokana na tatizo dogo tu linaloweza kutibika ikiwa wahusika wangejenga utamaduni wa kupata ushauri wa kiafya.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live