Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mama aliyejifungulia kwenye usalama

9358 Gaston+Nunduma1 TZW

Mon, 18 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Niliichukulia habari ya mama aliyejifungua kwenye kituo cha polisi mkoani Morogoro katika taswira mbili. Kwanza, nilihisi kuwa mtoto aliyezaliwa ni maalumu sana. Kwa Wakristo wanajua Biblia inavyoeleza jinsi wazazi wa Yesu walivyokosa nyumba hadi mama yake akajifungulia kwenye zizi la ng’ombe.

Lakini pili nilidhani kuwa mama huyo hakulielewa tangazo linalotolewa kila siku na Wizara ya Afya kwamba wajawazito wachukue tahadhari na kuhakikisha wanajifungulia “kwenye usalama”. Kwa muda mfupi nililipongeza Jeshi la Polisi kwa kurudisha imani kwa wananchi kiasi cha mama huyo kukimbilia kwao.

Katika miaka ya 1980 uliokuwa Muungano wa Nchi za Kisovieti (sasa Russia) ulisimamia vizuri usalama wa raia wake kupitia polisi. Ilifikia mahala Polisi walimsindikiza mlevi hadi mlangoni kwake bila kumsachi.

Katika miaka ile Warusi walikuwa wanapiga maji kwa kwenda mbele. Sijui ni sababu ya msongo au vipi, maana walikuwa Taifa kubwa lenye rasilimali watu kubwa na viwanda vingi, lakini nchi haikuwa na maendeleo kivile. Serikali yao iliwekeza kwenye nguvu za kijeshi kwa nia ya kuigeuza dunia nzima kuwa ya kikomunisti.

Raia walipiga kazi kwelikweli. Kulikuwa na viwanda vya ndege, meli na silaha nzito huko chini ya ardhi. Ndani ya siku moja mtu aliweza kufanya kazi katika viwanda vitatu na mwisho wa mwezi akapokea mishahara mitatu. Lakini kilichofuata baada ya mshahara ilikuwa pombe.

Wanaume hawakuwa na desturi ya kujenga familia. Walipopata pesa waliishia kwenye bustani za umma kulikouzwa pombe maarufu ya Vodka. Urusi (USSR) ilikuwa ikitoa ruzuku ya chupa ya Vodka kwa kila raia kwa ajili ya kujikinga na baridi kali. Raia wakajiongeza na mishahara yao na kufanya kila siku sherehe.

Akina mama walipoelemewa na mzigo wa familia wakagundua njia maridadi ya kuwabana waume zao.

Siku ya mshahara walikwenda kiwandani na kujipanga mistari miwili kushoto na kuume mwa geti pekee la kiwanda. Ilikuwa mfano wa jeshi linalokaguliwa na waheshimiwa.

Yeyote aliyemwona mumewe alimkamata na kwenda naye pembeni. Akamsachi na kumpukutisha fedha zote, kisha akamgawia fedha za kustarehe kwa siku tatu, akamwacha aende zake bustanini wakati yeye akienda kununua chakula, kulipa kodi na ada za watoto.

Kidume kilijifanya kulalamika, lakini mama alipopotea kilichomoa fedha kilizochimbia kwenye boksa na soksi, safari kwenda kuungana na wenzie kule bustanini ikafana.

Huko walilewa kuliko maelezo. Ulipofika usiku wa manane makarandinga ya polisi yalizungukia bustani zote na kuwakusanya walevi walioangusha bodi. Wakawapeleka vituoni ambako waliwasachi na kuwahifadhia pochi zao, kisha wakawalaza kwenye bwalo safi lenye vitanda vizuri. Asubuhi yake walevi waliitwa majina kulingana na vitambulisho vilivyokutwa kwenye pochi. Kila mmoja alirudishiwa fedha lakini baada ya kukatwa pesa ya malazi ya usiku uliopita. Wanaume wakalianzisha tena bustanini kupata supu na “kutoa loki”.

Hadithi hii ndiyo iliyonifanya niamini yule mama wa Morogoro alikwenda kujifungua mahali salama. Sikuweza kufikiria polisi eti wanaweza kumkamata mama mwenye ujauzito wa miezi tisa, tena si kwa tuhuma zilizomkabili binafsi, bali za mumewe.

Huwa natamani sana walinzi wa usalama wetu wafanane japo kidogo na wale wa Urusi ya zamani. Huwa siamini kabisa kama Warusi wametushinda utu na udugu tulionao Watanzania, ila ninachoamini ni wao kutushinda kielimu katika fani zao.

Nimesoma tangazo la ajira za Jeshi la Polisi kwa mwaka 2017/2018. Linawalenga vijana waliopo kwenye kambi za JKT/JKU ambao wamemaliza mafunzo ya awali katika Operesheni Kikwete na Operesheni Magufuli wenye elimu ya kidato cha nne, sita, astashahada, stashahada, stashahada ya juu na shahada.

Ni jambo jema kuwa na askari wenye elimu hasa katika wakati huu wa makuzi ya teknolojia. Bila shaka wakiongezea elimu ya kipolisi kule Moshi wanaweza kufanya kazi kwa weledi. Wanaweza kutazama, kupambanua na hatimaye kuamua si kuhukumu, bali kuamua wafanye lipi na waache lipi.

Nasema hivyo kwa sababu kuna uwezekano wa polisi kuingia lawamani kwa makosa yasiyokuwa yao. Enzi zile askari kanzu alikuwa ni polisi aliyevalia kiraia. Lakini alipomkamata mhalifu aliweza kujitambulisha. Hivi sasa kuna askari kanzu, polisi kidole na kadhalika. Katika tangazo lile sijaona polisi jamii inaingiaje. Jeshi liliamua kuwa na ulinzi shirikishi kwa nia njema ya kupunguza urefu wa daraja baina ya polisi na raia. Linamshirikisha raia kwenye ulinzi wa jamii yake na pia kutoa ushirikiano kwa jeshi kama raia mwema. Ikumbukwe kuwa wahalifu nao ni raia.

Napendekeza CCP (chuo cha polisi) wawe na vitengo kwa ajili yao. Nao wapewe elimu badala ya kuwaamini kwa sababu tu wanajua michongo ya mtaani na kuwapa pingu na rungu. Ujue kuwa ukimnunulia mwanao bunduki atacharaza wenzie kwa sababu hujamfundisha miiko yake.

Wapewe elimu na vitambulisho kiasi wanapokwenda kumkamata mtuhumiwa wajitambulishe, wamweleze nia yao na wamfikishe kunakohusika. Wafundishwe namna za ukamataji kwani kuna raia wanaotii sheria bila shuruti. Wakati mwingine matumizi ya pingu na rungu si ya lazima. Muwafunze tofauti ya matumizi ya nguvu ya chini, ya kati na ya juu. Kuku hachinjwi kama kitimoto ati!

Chanzo: mwananchi.co.tz