Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Malezi ya watoto yanahitaji sanaa

44655 Pic+malezi Malezi ya watoto yanahitaji sanaa

Tue, 5 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kile unachokipanda katika akili na ufahamu wa watoto wako leo, iwe kwa kujua au kutojua ndicho utakachokivuna pale watakapokuwa watu wazima.

Kama mzazi au mlezi kutowapatia taarifa bora na za kuwajenga, ulimwengu utakusaidia kazi hiyo kwa kuwapa taarifa zinazoweza kuwaharibu. Usifikiri kuwa kwa sababu uko kimya, hujawaambia kitu kuhusu mapenzi au tendo la ndoa inamaanisha hawajui kitu.

Wakati wote kazi ya kung’oa vile ulimwengu ulivyoviotesha kwenye akili na mioyo ya watoto huwa ngumu zaidi ya kazi ya sisi kuwapandia vilivyo vyema. Ndiyo maana ni rahisi kusikia sentensi kama hizi kuhusu malezi ya watoto; “Watoto hawa wamenishinda” “Nimeshanawa mikono” au “Nimekubali kushindwa”.

Siku zote fahamu kuwa maadili na nidhamu mtoto anayoipata nyumbani ni ya msingi na inadumu kuliko ile inayopatikana kokote kule.

Wote tutakubaliana na ukweli kwamba malezi ya watoto si kazi rahisi kama wengine wanavyoichukulia. Malezi ya watoto ni jukumu ambalo tunaweza kulibeba vyovyote tunavyotaka lakini tunapokuwa watu wazima au wazee tunafikia kujivunia jukumu hilo au kujilaumu kwa kushindwa kuwa wazazi au walezi bora. Nia yangu katika hili ni kujaribu kuchambua vitu vitakavyokusaidia na kukuwezesha kuja kujivunia utakapowaangalia wale uliowalea na kuwakuza jinsi wanavyofanyika mifano bora na kuleta sifa kwako au kwenu. Hakuna mzazi au mlezi anayetarajia au kungojea kuaibishwa na mtoto au watoto aliowalea mwenyewe, kila mzazi hata yule asiye na uhakika wa malezi yake anatarajia mema na kuwa na ndoto njema kuhusu watoto wake.

Hatua zitakazokusaidia

Kamwe usiwe na upendeleo kwa yeyote, fanya kila kitu kwa usawa pasipo kuonyesha upendeleo. Kumbuka kila mtoto ana vipawa au vipaji vyake vya tofauti na uwezo wao pia hutofautiana, vyote hivi havina budi kutambuliwa mapema utotoni na kupewa moyo au kuhamasishwa ili kuendelea, watoto wawezeshwe kuendeleza vile wanavyoonekana kuviweza mfano kipawa cha uimbaji, ufundi au michezo.

Epusha roho za mashindano baina ya watoto. Ushindani mdogo mdogo na wa kawaida hauna shida kwa sababu unaweza kuchochea kujibiidisha, tatizo ni yale mashindano yanayoweza kuleta ugomvi na uhasama, mara nyingi hili huonekana katika familia zenye watoto au mtoto wa baba peke yake au wa mama peke yake na wale wa wazazi wawili.

Wakati wote ondoa tofauti baina yao katika uhusiano wao ili usije kutengeneza ndugu ambao ni maadui watakapokuwa watu wazima.

Chochea ari ya kupenda shule na utamani wa kufaulu, kila mtoto ana kiwango cha juu cha uwezo ambacho kinatakiwa kutambuliwa.

Kama mwanao anaonekana kukosa hamasa ya shule aliyoko jaribu nyingine, fanya utafiti kwa kuzungumza naye nini anachokipenda katika elimu kwa sababu tafiti zinaonyesha kuwa mara nyingi masuala ya shule na elimu ni uamuzi wa lazima toka kwa wazazi peke yao pasipo watoto kuhusishwa au kushirikishwa.

Jaribu nyanja mbalimbali za elimu na usikate tamaa mapema. Jitahidi kuweka akiba ya fedha kwa ajili ya elimu ya watoto wako kwa sababu elimu ni bora lakini ni ya gharama na waswahili wamesema. “Ikiwa unaona elimu ni ghali basi jaribu ujinga”.

Penda kuwa na muda wakuzungumza na watoto wako, hususani wakati wa chakula cha jioni na zungumza nao mambo yaliyoendelea au yanayoendelea katika maisha yao kwa siku hiyo, watoto pia wanayo ya kukushirikisha, kwa namna hii watafurahi na kuongeza upendo na ukaribu kwa wazazi wao.

Kwa bahati mbaya tafiti zinaonyesha kuwa wazazi wa kiume hususani Wakiafrika hupata nafasi mara chache zaidi kula chakula cha jioni na familia zao.

Ikiwa ratiba yako ya usiku haikuruhusu basi jaribu kushiriki kifungua kinywa pamoja na watu wengine wa familia yako. Najua wako watakaojitetea kuwa ratiba zao hazikubali kabisa ila suala ni kwamba, ukiona umuhimu wa jambo hili basi utalifanya kuwezekana.

Kuza mazoea ya kifamilia yanayowaleta karibu zaidi kama vile kufanya na sherehe za krismasi au pasaka au sikukuu nyingine kwa pamoja nyumbani au kusafiri pamoja wakati huo.

Kukaribisha nyumbani kwenu marafiki wa mtoto au watoto wako siku za wikiendi au sikukuu.

Kuwaruhusu watoto kutoka kwa uangalizi maalumu. Huwezi kuelewa jinsi gani mambo haya yana umuhimu kwa mtoto wako mpaka apate tatizo fulani ndiyo utaelewa.



Chanzo: mwananchi.co.tz