Mwanza. Changamoto ya ukosefu wa mashine ya X ray lililokuwa likiikabili Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana jijini Mwanza, limepatiwa ufumbuzi baada ya Makamu wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kuahidi kuinunua.
Samia ametoa ahadi hiyo leo Jumapili Desemba 8, 2019 baada ya kuweka mawe ya msingi ya wodi ya wanaume na jengo la huduma ya uzazi ya mama na mtoto linalojengwa na Taasisi ya Maendeleo ya Aga Khan kupitia mradi wake wa Impact.
Ametoa mashine hiyo baada ya Mganga Mkuu wa Jiji la Mwanza, Juma Mfanga kusema wagonjwa wanapata taabu hivyo kusababisha foleni katika hospitali za Rufaa za Sekoutoure na Bugando.
“Hili la X ray limeisha, hivyo kamilisheni majengo inaletwa hapa mara moja,” amesema.
Pia, Suluhu amewasisitiza wananchi kuwa na bima ya Afya ili kuwarahisishia katika gharama za matibabu pindi wanapoumwa.
Amesema Serikali inajitahidi kuboresha huduma za afya hivyo wananchi nao wanawajibu kuipunguzia mizigo mzito.
Awali akitoa Meneja Mradi wa Impact Edina Selestine alisema jengo la hilo la mama na mtoto litagharimu Sh190. 6 milioni.
Amesema kulingana na uhaba wa wodi wazazi walikuwa wanazimika kulala watatu hadi wanne ambapo kwa mwezi hospitali hiyo inaweza kuzalisha 650.
Naye Dk Mfanga alisema jengo la wodi ya wanaume litagharimu Sh1. 4 bilioni ambalo litakuwa na uwezo wa kubeba vitanda 101.