Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Makamu wa Pili Z’bar atembelea majeruhi MOI

E5b8603a8c37fbc80797f518a28bfe44 Makamu wa Pili Z’bar atembelea majeruhi MOI

Thu, 24 Jun 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Hemed Suleiman Abdalla, amewatembelea majeruhi sita wa ajali ya basi iliyotokea mkoani Shinyanga Juni 2, mwaka huu.

Majeruhi hao kutoka Zanzibar ni wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Bugema cha Luwero nchini Uganda na wamelazwa katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), Dar es Salaam.

Wanafunzi hao walipata ajali wakati wakisafiri katika basi la Kampuni ya Classic wakitoka chuoni.

Katika ajali hiyo, watu wanne walipoteza maisha papo hapo na wengine kujeruhiwa wakiwemo wanafunzi hao waliopata majeraha makubwa ikiwa ni pamoja na kukatika mikono na miguu.

Akiwa hospitalini hapo jana, Abdalla aliwajulia hali majeruhi hao na kuwaeleza kuwa Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kwa pamoja zitahakikisha wanapata tiba ya hali ya juu na wanawaombea wapone haraka.

Baada ya kuwajulia hali, alisema ameridhishwa na huduma wanayopatiwa na madaktari na wauguzi wa MOI na kwamba wataendelea kutoa msaada utakaohitajika ili wanafunzi hao vijana wapone haraka na waendelee na masomo na kisha waje kuitumikia nchi yao. Wanafunzi hao ni wa shahada ya uuguzi.

“Nimekuja kuona hali zao, kwa kweli hali zao zinaendelea vizuri kwa maelezo yao wenyewe, nimefarijika kwa hilo kwani maelezo ya madaktari pia ni kwamba hali zao zinaendelea kuimarika. Nomeridhishwa na madaktari wanafanya kazi nzuri,” alisema Abdalla wakati akizungumza na HabariLEO.

Aliwaomba madaktari wasiharakishe kuwaruhusu mpaka wahakikishe afya zao ni nzuri na serikali ipo tayari kushirikiana nao kuhakikisha chamamoto zinatatuliwa ili wapone.

Akimpa maelezo kiongozi huyo mbele ya wagonjwa hao waliolazwa wodi namba 6A na 6B, Dk Victoria Munthali na muuguzi Florah Makundi, kwa nyakati tofauti walimueleza Makamu wa Pili wa Rais kuwa afya za majeruhi hao zinaimarika kila siku tangu walipowapokea Juni 4 na Juni 6, mwaka huu walipotolewa Shinganya na mmoja Hospitali ya Rufaa Bugando ya jijini Mwanza.

Majeruhi hao waliolazwa MOI ni Fatuma Kessy, Thwaiba Shaban Seif, Saada Mmanga Makame, Khalifa Rashid Abbas, Khadija Miraji Mohamed na Yahaya Mohamed Issa.

Saada alilieleza HabariLEO kuwa kulikuwa na ugumu wa safari hiyo tangu Kampala baadaye walifanikiwa kusafiri Juni Mosi na alfajiri ya Juni 2 ndio walipata ajali hiyo mkoani Shinyanga.

Alizishukuru serikali zote mbili (Muungano na Mapinduzi Zanzibar) kwa huduma walizopatiwa mpaka sasa wapo hai. Saada amekatika mkono wa kushoto na mguu.

Chanzo: www.habarileo.co.tz