Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maji ya moto kwa mama aliyejifungua hayana faida

62766 MAMA+PIC

Sat, 15 Jun 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ni jambo la kawaida kwa wazazi au walezi kutumia maji ya moto kuwakanda wanawake baada ya kujifungua.

Hata hivyo, ni wachache wanaojifungua kwa upasuaji ndiyo huwa hawakandwi, lakini wapo wanaokandwa.

Jamii hufanya hivyo kutokana na mazoea na tamaduni walizozikuta zinazoeleza kuwa unaweza kurejesha maumbile ya mwanamke ya asili kama ilivyokuwa kabla ya kujifungua kama tumbo na sehemu za siri kwa kumkanda na maji ya moto.

Kaimu Mratibu wa Huduma ya Afya ya Uzazi na Mtoto, Agnes Mgawa anasema mtindo wa kuwakanda na maji ya moto wanawake wakishajifungua ni hatari.

Mgawa amesema hayo wakati akizungumzia sababu za vifo vya wajawazito baada na wakati wa kujifungua katika mafunzo ya waandishi wa habari yaliyoratibiwa na Wizara ya Afya, shirika la kuhudumia watoto duniani (Unicef) na kampuni ya True vision production kupitia kampeni yake ya Jiongeze, Tuwavushe Salama.

Anasema kukandwa na maji ya moto kunaweza kusababisha mama kutokwa na damu nyingi na hata kifo.

Pia Soma

Kwa mujibu wa taarifa ya Voice of Amerika, daktari bingwa wa uzazi kutoka Cameroon, Dk Robinson Mbu anasema katika utafiti wa kitaalamu uliowahi kufanyika, ulibaini kuwa maji ya moto hayana umuhimu wowote kwa mzazi.

“Kunaweza kusababisha kizazi kutanuka na mama kutokwa na damu nyingi,” anasema Dk Mbu.

Katika hilo, Mgawa anaunga mkono akisema hawezi kushauri wanawake waliojifungua kukandwa maji ya moto japo suala hilo limezoeleka kwa wengi, lakini hakuna uthibitisho wa kitaalamu wa kumponya mwanamke kwa kutumia maji hayo isipokuwa kumletea madhara.

Daktari wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Denis Mugyabuso anasema kukanda maji moto ni asili tu iliyojengeka na isiyo na faida yoyote kitaalamu.

“Wito wangu ni kwamba mama anaweza kuoga kama kawaida alivyozoea,” anasema Dk Mugyabuso.

Jamii isemavyo

Hata hivyo, jamii inaamini maji ya moto ni tiba ya kurejesha maumbile ya asili kwa aliyejfungua. Kati ya wanawake watano niliozungumza nao, wote wanasema maji ya moto ni tiba japo hawana ushahidi wa kitaalamu.

“Nilijifungua kwa upasuaji nikaambiwa sitakiwi kukandwa kwa maji ya moto, mwezi mmoja baadaye (kidonda) kilianza kukauka, nikajikanda…maajabu damu zilitoka nikaacha kabisa kufanya hivyo(kukanda),” anasema Vaneria Kigamba, mmoja wa waliojifungua hivi karibuni.

Kigamba anasema alipata shida ile kwa sababu ya upasuaji aliokuwa amefanyiwa lakini anaamini maji ni tiba kwa sababu yanatumika tangu enzi za mababu.

Anitha Jedy, mkazi wa Mbezi Beach anasema aliwahi kupata tatizo la kutokwa damu baada ya kujifungua na kuanza kukandwa na maji ya moto.

“Mama mkwe alinikanda tumbo kwa maji ya moto sana na baada ya kukandwa nilishangaa kupata shida ya kutokwa damu kiasi kwamba ikabidi nirejeshwe tena hospitali,” anasema Jedy.

Bibi Ananikunda Kilima anasema walizoea kuona wanawake wakifanyiwa hivyo mila inayoendelezwa na wanafamilia wengi baada ya kujifungua. “Hata nilipokuwa msichana nilikandwa na nilikuwa naona afadhali nikifanyiwa hivyo, hii ni desturi yetu sisi wanawake hasa wa Afrika,” anasema Kilima.

Hata hivyo, Mgawa ambaye ni mratibu wa afya ya uzazi, anasema tiba hiyo haipaswi kuendelezwa kwa sababu mama anapaswa kuoga maji ya kawaida; na kulingana na maumbile yake, viungo vyake vitarejea kwenye hali ya kawaida vyenyewe.

Anasema kutokwa damu ni sababu moja tu kati ya sababu nyingi zinazoweza kusababisha vifo vya wanawake baada na wakati wa kujifungua.

Sababu hizo pia ndizo zinazowafanya watoto kuwa hatarini.

Takwimu za Wizara ya Afya zinaonyesha kuwa kati ya wanawake 556 kwenye vizazi hai 100,000 hufariki kutokana na uzazi. Mtaalamu wa mawasiliano kutoka Unicef, Usia Nkoma anasema sababu zinazochangia vifo hivyo zinaweza kuzuilika.

Sababu nyingine za vifo

Mgawa anataja sababu nyingine zinazochangia vifo baada na kabla ya kujifungua kuwa ni kifafa cha mimba, kuharibika mimba, uchungu pingamizi na upungufu wa damu.

Anasema mazingira yanayochangia kuwapo kwa vifo hivyo yanaweza kusababishwa na jamii kwa kutotimiza wajibu wake wa kuhakikisha mjamzito anawahishwa hospitali.

Pia, anasema sababu nyingine ni msongamano wa wagonjwa au wahudumu wachache baada ya kufikishwa hospitali.

“Asilimia 27 ya wajawazito wanaopokewa vituoni wapo kwenye umri mdogo na hawa wapo kwenye hatari ya kupoteza maisha kwa sababu kitaalamu na tunashauri walau mama abebe ujauzito kuanzia miaka 20 wakati nyonga zikiwa zimekomaa,” anasema Magava.

Anasema kihalisia mama akiwa kwenye hatari ya kupoteza maisha, mtoto pia anakuwa kwenye hatari hiyo.

Wajawazito kutopata huduma

Mgawa anataja sababu za wanawake wajawazito kutopata huduma za kiafya kuwa ni pamoja na umbali kutoka kwenye makazi mpaka hospitali, hali duni ya maisha, ukosefu wa elimu na mila na desturi pingamizi.

Anasema sababu nyingine ni upungufu wa watoa huduma wenye ujuzi, upungufu wa dawa na vifaa tiba sambamba na ushirikishwaji mdogo wa wanaume kwenye masuala ya uzazi.

“Mfano tu kuna mama alikuja hospitali kwenye kliniki ya kawaida akaambiwa anapaswa kubaki hospitali alazwe kwa sababu anashida ya kifafa, kwa sababu tu hakumuaga mumewe mama yule alipolazwa alitoroka kurudi nyumbani,” anasimulia.

Anasema muda mfupi baada ya kurudi hali yake ilibadilika na hospitali alipotafutwa hakuwepo.

“Hali ilikuwa mbaya kiasi kwamba kitendo cha kuhangaikia usafiri hadi kumfikisha hospitali alikuwa ameshapoteza maisha yake,” anasema.

Nini kifanyike?

Nkoma wa Unicef anasema usalama na uhai wa mjamzito kabla na baada ya kujifungua unagusa nyanja nyingi.

“Kwanza kabisa suala la kuzaa halipaswi kuwa jambo la kufa na kupona, mjamzito hapaswi kuwa na hofu yoyote kuhusu uhai wake, eneo hili lazima tupige hatua ili kuokoa uhai wa mama na mtoto,” anasema Nkoma.

Pia, anashauri jamii ipatiwe elimu kuhusu uzazi hasa kuwawahisha wajawazito hospitali ili wapate huduma stahiki.

“Hata hili la maji ya moto jamii ifundishwe kuwa halina faida yoyote zaidi ya madhara, kiafya siyo sahihi kabisa. Mama aoge maji ya kawaida tu aliyozoea,” anasema.

Anashauri Serikali kuendelea kuongeza bajeti ya wizara ya afya ili kuimarisha huduma ya mama na mtoto kwenye vituo vyote vya afya na zahanati.

“Lakini wahudumu kila wakati wawe wanapewa mafunzo mahususi, Serikali ihakikisha kunakuwa na vifaa muhimu,” anasema Nkoma.

Mkakati wa Serikali

Mgawa ambaye ni mratibu wa afya ya uzazi anasema mkakati uliopo ni kuhakikisha vifo vya wajawazito baada na kabla ya kujifungua vinapungua hadi kufikia 292 katika kila vizazi hai 100,000.

Hata hivyo, wakati akifungua jengo la huduma za Afya Binafsi katika Hospitali ya CCBRT, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,= Ummy Mwalimu anasema kwa kushirikiana na wadau vifo vya wajawazito vimepungua.

Anasema awali, vifo vilikuwa vingi kutokana na kukosekana kwa huduma lakini sasa Serikali imejenga vituo vya afya 350 ikiwa ni pamoja na kuweka huduma za dharura ya kumtoa mtoto tumboni.

Chanzo: mwananchi.co.tz