Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maji baridi ni sawa kabla na baada ya mazoezi?

46125 PIC+MAJI Maji baridi ni sawa kabla na baada ya mazoezi?

Mon, 11 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kwa mwanamichezo yeyote kunywa maji mengi yakutosha kabla na baada ya mazoezi ina faida kubwa kiafya kuzuia na kurudishia maji na chumvi chumvi vilivyopotea kwa njia ya jasho.

Inapotokea mwanamichezo amepata upungufu wa maji mwilini anaweza kukumbana na madhara mbalimbali ya kiafya ikiwamo kukamaa misuli, kukosa umakini na kupoteza fahamu uwanjani kusababisha.

Kumekuwa na mijadala mbalimbali kuhusu ni maji gani yanafaa kunywa kabla au baada ya mazoezi, yaani kati ya maji yenye baridi au ya vuguvugu au ya kawaida.

Ni kawaida kabisa kumwona mwanamichezo aliyetoka katika mazoezi akitamani zaidi kunywa maji baridi sana kuliko ya vuguvugu au ya kawaida.

Utafiti mbalimbali wa kitabibu unaonyesha kuwa maji ya kawaida au ya vuguvugu ndiyo yanafaida kubwa kiafya kuliko maji baridi, hii ni kwa sababu mwili unahitaji kufanya kazi kubwa ya kunyanyua joto la maji baridi yaliyoingia katika mfumo wa chakula ili yaweze kufyonzwa.

Mwili huwa na joto lake la wastani ambalo vimeng”enya (enzymes) na vitu vingine vya mwilini huweza kufanya kazi yake yakuwezesha maji kunyonywa kwa haraka na kwa urahisi.

Hivyo kwa sababu hii maji ya kawaida au vuguvugu ndiyo yanafaa zaidi kunywa baada ya kufanya mazoezi kwani yananyonywa haraka zaidi kuliko ya baridi.

Ikumbukwe baada ya mazoezi mwili unakuwa umepoteza maji hivyo kunakuwa na uhitaji wa maji mengi ili kurudishia maji yaliyopotea kwa njia ya jasho.

Hali hii yakupoteza maji inawahusu zaidi wanamichezo ambao wanacheza katika maeneo yenye joto kali zaidi.

Wapo baadhi ya wafanya mazoezi ambao wanatumia njia ya kunywa maji baridi baada ya kucheza au mazoezi kama njia ya kukabiliana na unene.

Ni kweli kitaalam inakubalika kunywa maji ya baridi sana inasaidia kuchoma nishati (mafuta) ya ziada ya mwili kwani mwili utahitaji kutumia nguvu kubwa zaidi ili kupandisha joto la maji hayo ya baridi. Bado njia hii si madhubuti katika kukabiliana na unene ukilinganisha lishe na mazoezi mepesi.

Hivyo ni sahihi zaidi kwa wanamichezo kutumia maji ya kawaida au vuguvugu na kunywa kabla au baada ya kumaliza mazoezi kwani yana faida kubwa kiafya kulinganisha na maji ya baridi ambayo mwili huchelewa kuyafyonza.

Ingawa ieleweke pia kwa atakayekunywa ya baridi hawezi kupata madhara bali atakosa faida ya maji hayo kunyonywa kwa haraka mwilini.



Chanzo: mwananchi.co.tz