Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Majaliwa atoa siku 15 kukamilisha ujenzi hospitali ya Uhuru

5636800d09c8298ed0bc74fe093ba6a9.png Majaliwa atoa siku 15 kukamilisha ujenzi hospitali ya Uhuru

Sat, 21 Nov 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa siku 15 kwa uongozi ya Wilaya ya Chamwino, Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) na Suma JKT wahakikishe ujenzi wa hospitali ya Uhuru katika Halmashauri ya Chamwino unakamilika.

Akizungumza baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa hospitali hiyo, Waziri Mkuu alisema lengo ni kuhakikisha hospitali hiyo inazinduliwa na Rais John Magufuli ifikapo Desemba 9, mwaka huu ili kutimiza maono yake ya ujenzi wa hospitali hiyo.

"Nimeridhika na hatua hii ya ujenzi lakini haitoshi, hamieni hapa, huu ni wakati wa kazi, hakikikisheni kazi inafanyika usiku na mchana ili Desemba 5, 2020 kazi ikamilike na Desemba 9, 2020 izinduliwe," alisema Majaliwa.

Alisema anataka kuona vifaa vyote vya ujenzi wa hospitali hiyo vinatoka kwenye viwanda vya ndani kuharakisha ukamilishwaji wa hospitali hiyo hasa marumaru kwani nchi inavyo viwanda vikubwa vinavyozalisha bidhaa hiyo kwa ubora wa hali ya juu.

"Mnabishana kuhusu uwekaji wa tiles (marumaru), mnataka za nje? TBA mnang'ang'ania kununua tiles kutoka nje ya nchi, kwa nini? Sisi tumehamasisha ujenzi wa viwanda na viwanda vipo vinavyotengeneza tiles tena nzuri,” alisema.

Alisisitiza, “Tuna kiwanda Chalinze kikubwa sana na kingine kipo Mkuranga, hata jengo letu la Tume ya Taifa ya Uchaguzi tumeweka tiles za ndani, na bora mshitiri hujazinunua, na usinunue kutoka nje, tuna viwanda vipo nchini."

Akitoa taarifa ya ujenzi wa hospitali hiyo, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais (Tamisemi), Joseph Nyamhaga alisema kuwa ujenzi wa hospitali hiyo ni utekelezaji wa agizo la Rais Magufuli alilotoa kwamba Sh milioni 995.1 zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya maadhimisho ya miaka 57 ya Uhuru mwaka 2018 zitumike katika ujenzi wa hospitali hiyo.

Pia, Januari 2019, wakati akipokea gawio la hisa za kampuni ya simu ya Airtel, aliagiza Sh bilioni 2.415 zitumike kwenye ujenzi huo.

Alisema hadi Novemba 19, mwaka huu, Sh 4,430,721,498.00 zilipokewa kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo. Alisema 4,062,310,051.76 zimeshatumika na ambazo hazijatumika ni Sh 368,411,446.24.

Akieleza mipango ya baadaye, Nyamhanga alisema mwaka 2020/2021, Serikali imepanga kuendelea na ujenzi wa hospitali za halmashauri 27 ambazo kila moja imetengewa sh. bilioni moja.

Aidha, alisema Sh bilioni 27.75 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa zahanati 555 ambapo zahanati tatu zitajengwa kwa kila halmashauri na kila moja inagharimu Sh milioni 50.

Msaidizi wa Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa, Kanali Laurence Lukema alisema wao kama wakandarasi wa ujenzi, watahakikisha ujenzi wa hospitali hiyo unakamilika kwa wakati.

Chanzo: habarileo.co.tz