Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali inaendelea kuboresha huduma mbalimbali za kijamii nchini zikiwemo za afya, na hivyo kuwataka Wananchi kuendelea kuipa ushirikiano.
Majaliwa ameyasema hayo wakati akizungumza na Wananchi baada kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Newala akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Mtwara.
Pia, Waziri Mkuu amemuagiza Mkuu wa wilaya ya Newala asimamie ipasavyo upatikanaji wa dawa katika vituo vya kutolea huduma za afya kwa sababu Serikali inatoa fedha nyingi kwa ajili ya kugharamia huduma hiyo.
Amesema Serikali kila mwezi inapeleka fedha kwa ajili ya ununuzi wa dawa, hivyo hatarajii Wananchi wanaokwenda kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kukosa dawa.
Waziri Mkuu amesisitiza dawa zipelekwe wilayani Newala kulingana na magonjwa yanayopatikana katika wilaya hiyo.
Awali, Mganga Mkuu wa wilaya ya Newala Dkt. Matiko George alisema Serikali imetoa shilingi Bilioni 2.85 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali likiwemo jengo la maabara, wagonjwa wa dharura, huduma ya mama na mtoto, mionzi, utawala, wodi za wanawake, wanaume na watoto.