Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Majaliwa: Tumedhamiria kuboresha huduma za afya nchini

24900 Pic+majaliwa TanzaniaWeb

Thu, 1 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Lushoto. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali imedhamiria kuboresha huduma za afya kwenye maeneo mbalimbali nchini yakiwemo ya halmashauri ya wilaya ya Lushoto.

Amesema lengo ni kuhakikisha kila kata inakuwa na kituo cha afya chenye uwezo wa kutoa huduma mbalimbali muhimu zikiwemo za maabara, upasuaji na mama na mtoto.

Ametoa kauli hiyo leo Jumatano, Oktoba 31, 2018 wakati akizungumza na wananchi wa kata ya Malindi baada ya kutembelea jengo la soko la mbogamboga la Malindi.

Waziri Mkuu amesema Serikali imejipanga vizuri katika sekta ya afya baada ya bajeti ya kununulia dawa kuongezeka kutoka Sh31blioni kwa mwaka na kufikia Sh269bilioni.

“Hatutaki tena kusikia mgonjwa anaenda hospitali na kukosa dawa biashara hiyo tumeimaliza, Rais Magufuli (John) ametoa fedha nyingi kwa ajili ya ununuzi wa dawa,” amesema.

Amesema katika wilaya ya Lushoto, Serikali imetenga Sh1.4bilioni kwa ajili ujenzi na ukarabati wa majengo ya vituo vya afya vya kata za Kangagai, Mnazi na Mlola.

“Halmashauri wekeni mpango thabiti wa kujenga wodi mbili kati yake moja ya wanaume na nyingine ya wanawake, lengo la Serikali ni kuboresha huduma za afya kwa wananchi,” amesema Majaliwa.

Akizungumzia kuhusu mradi wa ujenzi wa soko, Majaliwa amesema mradi huo ni sehemu ya huduma zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya kuboresha huduma za jamii nchini.

Waziri Mkuu ametaja huduma nyingine zinazotolewa na Serikali kwa wananchi kuwa ni afya, elimu, maji, uchumi, ujenzi na uboreshwaji miundombinu mbalimbali ikiwemo ya barabara.

Amewataka wananchi watumie vizuri soko hilo ambalo linatoa fursa kwao kufanya biashara katika eneo zuri na kuwawezesha kuuza bidhaa zao zikiwa katika ubora.

Pia amewashauri wakulima hao wajiunge katika vikundi na kuanzisha ushirika wao ili waweze kusaidiwa na Serikali katika kupata mikopo kwa ajili ya kuzalisha kwa ubora zaidi.

Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Lushoto, Ikupa Mwasyoge amesema kukamilika kwa soko hilo kutainufaisha halmashauri na wananchi.

Ikupa amesema ujenzi wa jengo hilo la soko la ghorofa mbili lililojengwa kwa awamu mbili ulianza mwaka 2011 na kukamilika Septemba 2018 kwa gharama ya Sh1.1bilioni.

Amesema halmashauri itanufaika kwa kupata ushuru na wananchi ambao wengi wao ni wakulima wa mboga na matunda watakuwa na sehemu ya uhakika ya kufanyia biashara.

“Wakulima 35,000 wa kata ya Malindi na kata jirani za Lukozi, Manolo na Shume wanaozalisha wastani wa tani 5,900 za mboga na matunda kwa mwaka watanufaika,” amesema.

Kwa upande wake Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema Serikali imefanya kazi kubwa kuboresha huduma za afya nchini.

Amesema bajeti ya dawa katika halmashauri hiyo imeongezeka kutoka Sh183mlioni za dawa zilizokuwa zinatolewa awali na sasa imefikia Sh565milioni.

Mbunge wa Mlalo (CCM), Rashid Shangazi ametumia fursa hiyo kuishukuru Serikali kwa kuwasaidia wananchi wa halmashauri kuongeza thamani ya mazao yao kabla ya kuuza.

Awali, Majaliwa alizindua jengo la utawala la halmashauri ya wilaya ya Lushoto lililogharimu Sh4.3bilioni.

Chanzo: mwananchi.co.tz