Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Majaliwa: AKDN, NHIF mjadiliane

60228 Pic+majaliwa

Thu, 30 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameutaka uongozi wa Taasisi ya Maendeleo ya Aga Khan (AKDN), kukamilisha majadiliano na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ili watumiaji wa bima zake waweze kutibiwa katika hospitali za Aga Khan.

Kauli hiyo ilitolewa jana wakati Majaliwa alipokutana na viongozi wa AKDN na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, ofisini kwake bungeni jijini Dodoma.

Majaliwa alisema Serikali inatambua mchango unaotolewa na AKDN katika kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya hapa nchini.

Aliwapongeza viongozi hao kwa utoaji wao wa huduma kwenye sekta nyingine kama elimu, maji na kilimo.

“Tunategemea mtaendelea kuimarisha huduma hizo ili ziwasaidie Watanzania wengi zaidi,” alisisitiza.

Viongozi hao walikutana na Waziri Mkuu ili kumuarifu juu ya mpango wa taasisi hiyo kuanzisha kituo maalumu cha matibabu ya saratani nchini ambao unatarajiwa kugharimu dola za Marekani milioni 15.9 (zaidi ya Sh34 bilioni).

Pia Soma

Kituo hicho kitaendeshwa kwa ubia baina ya hospitali za Ocean Road, Muhimbili, Bugando na Aga Khan.

Awali, akitoa maelezo kuhusu mpango wa kujenga kituo hicho, Mwakilishi Mkazi wa AKDN nchini, Amin Kurji alisema wameshawasiliana na hospitali zote tajwa na sasa wanashirikiana na wataalamu wa Wizara ya Afya ili kukamilisha suala hilo.

“Tatizo la saratani hapa nchini ni kubwa kwa sasa. Lakini tunataka watu watambue kwamba ukiugua saratani haimaanishi kwamba ni adhabu ya kifo. Inaweza kutibika endapo mgonjwa atawahi kupata matibabu,” alisema Kurji.

Alisema kwa sasa hapa nchini hakuna kituo maalumu cha matibabu ya saratani lakini kitu cha pekee kuhusu kituo hicho ni uwapo wa huduma zinazotembea za upimaji na utoaji tiba hadi mikoani.“Huduma hizi zitakuwa zinatolewa kwenye mikoa yote kupitia njia ya mtandao, ilhali vituo vikuu vya Dar es Salaam na Mwanza vitakuwa vikitoa majibu kwa madaktari husika,” alisema Kurji.

Alisema lengo ni kutoa elimu juu ya kuzuia, upimaji wa mapema na upatikanaji wa tiba.

Chanzo: mwananchi.co.tz