Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maiti ya kichanga yafikisha siku 40 mochwari kusubiri DNA

Sun, 18 Oct 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mgogoro kati ya uongozi wa kituo cha afya Nguvu Kazi kilichopo Nyeburu, Chanika mkoani Dar es Salaam na wazazi umesababisha maiti ya mtoto mchanga kukaa mochwari kwa siku 40.

Mgogoro huo ulianza baada ya mama wa mtoto huyo Maisha Ally kujifungua Septemba 7 kituoni hapo na kupewa taarifa kuwa mtoto wake alipelekwa hospitali ya Amana na kisha kufariki dunia wakati akipata matibabu.

Kufuatia kauli hiyo Maisha na mumewe Stephano Alphonce walikilalamikia kituo hicho kuwa kimeuza mtoto wao na kuamua kuisusa maiti hiyo inayodaiwa kuwapo hospitali ya Amana hadi kufanyike uchunguzi wa vinasaba (DNA).

Kufuatia malalamiko hayo Septemba 15 Serikali iliunda kamati ya kuchunguza utata huo ambayo ilianza kwa kuwahoji wazazi wa mtoto huyo na watumishi wa kituo.

Baada ya kamati kufanya uchunguzi, Oktoba Mosi mwaka huu ilijiridhisha kuwa kuna ulazima wa kupima vinasaba vya mtoto huyo na wazazi wake yaani ili kujiridhisha zaidi.

Akizungumza na Mwananchi jana, Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala Jumanne Shauri alisema bado uchunguzi unaendelea na watatoa majibu pindi utakapokamilika.

Pia Soma

Advertisement
“Tume iliyoundwa inaendelea na uchunguzi na bado taratibu za uchukuaji na upimaji wa vinasaba unaendelea, hivi karibuni tutatatua suala hilo,” alisema Shauri.

Akizungumza nyumbani kwake Septemba 14, Maisha alisema waliisusa maiti hiyo kwa kuwa utaratibu wa mtoto kuhamishwa hospitali haukufuatwa na kulikuwa na udanganyifu wakati wa mchakato wake wa kujifungua.

Tofauti na utaratibu ulivyo, Maisha alidai alipojifungua hakuonyeshwa mtoto, wala kuambiwa amejifungua jinsia gani, lakini ndugu zake walipokea taarifa kutoka kwa wauguzi kuwa alipojifungua alipoteza fahamu ilhali yeye akidai kuwa alichomwa sindano ya ganzi pekee na alikuwa na fahamu.

“Nilijifungua Septemba 7 saa saba mchana kwa njia ya upasuaji kwa kuchomwa sindano ya ganzi mgongoni. Wakati wa upasuaji ilikuwa kimyakimya sikuambiwa chochote wala kuonyeshwa mtoto. Baadaye saa 10 ndugu walikuja na shangazi aliingia nikaongea naye, ila niliona anashtuka,” alisimulia Maisha.

Chanzo: mwananchi.co.tz