Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Magufuli kuweka jiwe la msingi Hospitali ya Rufaa Njombe

51345 Pic+njombe

Wed, 10 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Siku moja kabla ya Rais John Magufuli kuweka jiwe la msingi ujenzi wa Hospitali ya Mkoa wa Njombe, Tanzania imeelezwa kufanikiwa kuvuka kiwango cha upatikanaji dawa muhimu kwa binadamu kilichowekwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) katika ngazi ya hospitali za wilaya.

Hospitali za wilaya zimekuwa na idadi kubwa ya dawa muhimu zinazopatikana kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kufikia dawa 312 wakati kigezo kilichowekwa na WHO ni dawa 300.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu katika ziara yake mkoani Njombe alipotembelea Hospitali Teule ya Rufaa ya mkoa huo kujionea hali ya utoaji wa huduma.

Waziri Ummy aliyeongozana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk Zainab Chaula pamoja na watendaji walio chini ya wizara yake, amesema kuwa Serikali ya awamu ya tano imeendelea kuboresha upatikanaji wa dawa kwa wananchi huku ikipitiliza kiwango kilichowekwa na WHO kwa kuwa na dawa muhimu 312.

“Tuna mfumo wa ukusanyaji wa taarifa kuanzia ngazi ya zahanati, kituo cha afya mpaka hospitali unaotuwezesha Serikali kutambua mahitaji na matumizi ya dawa katika vituo vya kutolea huduma,” amesema Waziri Ummy wakati akifafanua namna ya Serikali ilivyojipanga kupata takwimu sahihi za dawa.

Amezitaja dawa zenye kipaumbele kikubwa zikiwemo za kudhibiti maambukizi ya bakteria (Antibiotics), malaria, magonjwa yasiyo ya kuambukiza, uzazi salama pamoja na dawa za maumivu.

Related Content

Kwa upande wake katibu mkuu Wizara ya Afya Dk Zainab Chaula amesema kuwa ofisi yake kupitia Waziri wa Afya wako mbioni kuwasilisha muswada wa Bima ya Afya ambao utawawezesha wananchi wote sasa kuwa na bima ya afya.

Amewataka watumishi wa hospitali hiyo kuwahamasisha zaidi wagonjwa kujiunga na huduma za bima ya afya ili kuwa na uhakika wa matibabu pindi wanapougua.

“Niwaombe watendaji wote hapa kuwasisitiza wagonjwa wanaofika kupata matibabu kujiunga na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya,” amesema Dk Chaula.

Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo Dk Winfred Kyambile amesema hali ya upatikanaji wa huduma imeimarika kutokana na mapato kuongezeka hivyo kuiwezesha hospitali kutoa huduma bora kwa wananchi.

Dk Kyambile amesema kuongezeka kwa upatikanaji wa dawa imesaidia kuongezeka kwa mapato hospitalini hapo, amesema kuwa hapo awali mapato ya hospitali hiyo kwa mwezi yalikuwa Sh 12 milioni huku sasa mapato hufikia Sh90 mpaka 100 milioni, fedha ambazo amesema wanazitumia kuboresha huduma za afya katika hospitali hiyo.



Chanzo: mwananchi.co.tz