Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Magufuli atoa miezi 2 ujenzi hospitali ya wilaya

1301af43d6a1910c1ea9cda271636bb9.jpeg Magufuli atoa miezi 2 ujenzi hospitali ya wilaya

Wed, 2 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MGOMBEA urais wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) John Magufuli ameuagiza uongozi wa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida uhakikishe ndani ya miezi miwili kuanzia sasa ukamilishe ujenzi wa hospitali ya wilaya hiyo.

Amesema Novemba mwaka huu ataenda kuizindua ili huduma za tiba zikiwemo za upasuaji zianze kutolewa kwa wananchi.

Alitoa agizo hilo jana wilayani hapo aliposimama kuomba kura kwa wananchi wakiwemo wa majimbo ya Singida Mashariki na Magharibi.

Aliomba kura hizo wakati akiwa njiani kwenda Singida mjini kufanya kampeni kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu zilizoanza Agosti 26 mwaka huu.

Magufuli alisema wananchi wanataka huduma bora za kijamii, afya, elimu , maji na nyingine hivyo amemuagiza Mkuu wa Wilaya hiyo, Edward Mpogolo asimamie ujenzi wa hospitali hiyo ukamilikie ndani ya mezi miwili.

“Viongozi wote wa wilaya wako hapa hata wa mkoa, sasa pamoja na kwamba niko kwenye kampeni lakini naagiza, Mkuu wa Wilaya simamia hili la ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Ikungi ndani ya miezi miwili iwe imekamilika, nitakuja kuifungua Novemba , wananchi watibiwe wapate huduma za upasuaji na dawa” alisema.

Aliagiza kama kuna mkandarasi amesimama kwenye ujenzi huo, uongozi wa wilaya uhakikishe wanaanza kazi mara moja na kama kuna tatizo la fedha, lisemwe kwani serikali ni tajiri.

“Serikali ni tajiri, kama kuna tatizo la pesa katika ujenzi wa hospitali hiyo, semeni, na kama kuna mkandarasi alisimama arejee kazi ziendelee,”alisema Magufuli.

Alisema ujenzi wa hospitali hiyo unagharimu shilingi bilioni 1.5, na kwamba, utekelezaji wake umo pia ndani ya Ilani ya CCM.

Awali, akizungumza na wananchi wa Ikungi, mgombea ubunge wa Jimbo la Singida Mashariki, Miraji Mtaturu (CCM), alimshukuru Magufuli kwa kuhakikisha fedha za miradi zilizoombewa katika jimbo hilo zimetolewa.

Mtaturu alisema hadi sasa ujenzi wa majengo manane ya hospitali ya wilaya ya Ikungi umefika kwenye lenta na wanategemea Januari mwakani uwe umekamilika.

Mgombea ubunge Jimbo la Singida Magharibi, Elibariki Kingu (CCM), alimhakikishia Magufuli atashinda uchaguzi wa Rais kwa sababu ya kazi alizofanya zilizoacha alama.

Chanzo: habarileo.co.tz