Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Magonjwa yasiyoambukiza tishio la kiafya

C79e9beab92e77dd435152963775fa15.jpeg Magonjwa yasiyoambukiza tishio

Sat, 11 Dec 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo kisukari, shinikizo la damu na saratani yametajwa kuwa ni miongoni mwa magonjwa ambayo ni tishio kwa jamii, kutokana na jamii kutokubadili mtindo wa maisha ikiwemo lishe.

Hayo yalibainishwa na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro ya Mawenzi, Dk Edina-Joy Munisi, wakati wa kilele cha maadhimisho ya wiki ya Mawenzi, yaliyoenda sambamba na kuadhimisha miaka 60 ya Uhuru, katika viwanja vya Uhuru Park, mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro.

Alisema kwa sasa magonjwa yasiyoambukiza yamekuwa tishio kubwa kwa jamii, hatua ambayo imekuwa ikichangiwa na mtindo wa maisha ikiwemo watu kutofuata taratibu za afya ikiwemo lishe, jambo ambalo halipaswi kupuuzwa.

Katika wiki ya Mawenzi na maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara, hospitali hiyo ilitoa matibabu na vipimo bure kwa watu zaidi ya 4,000.

“Utaratibu tuliouanzisha wa utoaji wa matibabu na uchunguzi wa magonjwa ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha miaka 99 ya Mawenzi na miaka 60 ya Uhuru wa nchi yetu, tumebaini kuwa jamii inakabiliwa na tatizo kubwa la magonjwa yasiyoambukiza kama sukari, shinikizo la damu na saratani,” alisema.

Alisema ni wajibu wa jamii kubadili mtindo wa maisha kwa usalama wa afya zao ambapo mbali na kuhakikisha watu wanazingatia lishe bora, wanatakiwa pia kuacha tabia ya matumizi holela ya dawa kabla ya kufanya vipimo ambayo yamekuwa yakisababisha magonjwa. Alisema wananchi pia wanatakiwa kudumu na mazoezi.

Aidha, alisema kati ya wananchi zaidi ya 4,000 waliofika na kufanyiwa uchunguzi wa magonjwa mbalimbali, 400 walibainika kuwa na matatizo ya magonjwa hayo yasiyoambukiza na kuanza kupatiwa matibabu.

“Tulipata mwitikio mkubwa kwa wananchi ambapo walijitokeza na tuliwapatia vipimo vya magonjwa ya tezi dume, saratani ya shingo ya kizazi pamoja na kupata chanjo ya homa ya ini,” alisema.

Kwa upande wake, Dk Grace Temba, kutoka Idara ya Macho ya hospitali hiyo, alisema mbali na magonjwa yasiyoambukiza pia magonjwa ya macho yameendelea kushamiri kwa wananchi kutokana na elimu duni na ukosefu wa huduma za matibabu katika maeneo ya vijijini.

Evance Mlay, ambaye ni miongoni mwa wananchi waliopata huduma katika viwanja hivyo, alisema wamenufaika na matibabu na uchunguzi uliofanywa bure kwa wananchi.

Alisema suala hilo ni vema likawa endelevu kutokana na ukweli kwamba wananchi wengi wamekuwa wakishindwa kumudu gharama za matibabu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live