Serikali kupitia Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema Magonjwa yasiyo ya kuambukizwa kama moyo,figo na mengineyo yanaongezeka kwa kasi duniani kote na hapa nchini yamekua yakigharimu Serikali kiasi cha shilingi Bilioni 36.6 kwa mwaka.
Hayo yamesemwa na Waziri Ummy, wakati wa uzinduzi wa bodi ya wadhamini ya Hospitali ya Benjamin Mkapa Jijini Dodoma.
Waziri Ummy amesema hapa nchini kwa takwimu za Julai 2013 hadi Juni 2016 magonjwa ya Moyo na Figo ndiyo yalikuwa yakiongoza kwa idadi kubwa ya wagonjwa kutibiwa nje ya nchi na kugharimu Serikali kiasi hicho cha fedha.
“Kati ya wagonjwa 560 waliosafirishwa na Serikali wagonjwa 430 walienda kutibiwa moyo na wagonjwa 160 walienda kupandikizwa figo ”alisema Ummy.
Aidha, Waziri Ummy alisema kuwa kwa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) magonjwa yasiyoambukiza yanachangia vifo kati ya watu mia moja watu sitini hufa kwa magonjwa hayo na kati ya wagonjwa 100 watu 47 wanaugua magonjwa yasiyoambukiza
Waziri Ummy aliongeza kuwa kwa kuanzishwa hospitali ya Benjamin Mkapa kutaokoa kiasi kikubwa cha fedha na kuipunguzia Serikali mzigo mkubwa wa gharama na badala yake fedha hizo zitatumika kuimarisha miundombinu ya hospitali za hapa nchini.
“Nawaomba mkachape kazi bila kuchoka ili hospitali hii ikawe na tija katika kuwahudumia watanzania na hata ndugu zetu wa nchi jirani hasa za Jumuiya ya Afrika Mashariki katika huduma za matibabu ya Kibingwa”,Alisisitiza Waziri Ummy.