Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Magonjwa ya figo yageuka mzigo mifuko ya bima

Figoo (600 X 400) kati ya wagonjwa 2,750 ni 250 pekee ambao hawapo katika mfumo wa bima ya afya.

Thu, 21 Apr 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Imeelezwa kuwa kati ya wagonjwa 2,750 wanaopata huduma ya uchujaji wa damu kupitia mashine maalumu ‘dialysis’ ni 250 pekee ambao hawapo katika mfumo wa bima ya afya.

Magonjwa ya figo yametajwa kutumia kiasi kikubwa cha fedha za Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ikilinganishwa na magonjwa mengine huku kukiwa na ukuaji wa kasi wa matumizi kila mwaka.

Idadi hiyo kubwa imetajwa kuongeza mzigo mkubwa kwa mifuko ya bima mbalimbali, kutokana na kutumia kiasi kingi cha fedha kulipia huduma za matibabu ya uchujaji damu.

Hayo yamesemwa na Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Aifelo Sichwale wakati akifungua mkutano wa viongozi wa vyama vya kitaaluma nchini uliozungumzia uboreshaji wa huduma za afya nchini, uwajibikaji na maadili ya watumishi wa afya.

“Suala la magonjwa yasiyoambukiza limekuwa na changamoto kubwa ni sehemu wataalamu mlifanyie tafiti ili tutoke huku tuliko, leo hii kati ya wagonjwa 2750 wa dialysis 250 kati yao ndiyo hawapo katika mfumo wa bima.

“Hapa unaona ni namna gani mifuko ya bima inaumia fedha nyingi zinakwenda kutibu magonjwa sugu, wataalamu mliwekee mpango madhubuti, fanyeni tafiti ambazo Serikali zitatusaidia kufanya maamuzi si huko tu hata katika masuala ya Uviko-19 na kwingineko,” amesema Dk Sichwale.

Aidha katika hatua nyingine Dk Sichwale ametilia mkazo suala la upotevu na uharibifu wa dawa unaofanywa kwa kutozingatia mwongozo.

“Hapa tumechafuka sana ukiangalia suala la dawa ripoti zake zinatisha. Huko vituoni hakuna maoteo ya dawa, hakuna wa kupokea dawa, kamati zipo lakini hazikai, kutunza dawa bado ni shida kubwa,” amesema.

Mkurugenzi wa huduma za wanachana wa mfuko huo, Christopher Mapunda amesema mwenendo wa ukuaji wa gharama za matibabu kwa magonjwa hayo imeongezeka.

“Matibabu ya figo kwa mwaka 2017/18 zilikuwa Sh16.54 bilioni sawa na asilimia 62 huku 2018/19 Sh20.51 bilioni sawa na asilimia 24.

“Mwaka 2019/20 mwenendo wa gharama za matibabu ya figo zilikuwa ni 27.16 bilioni sawa na ukuaji asilimia 32 huku mwaka 2020/21 zikiwa Sh32.89 bilioni sawa na ukuaji wa asilimia 21.

Mapunda amesema mfuko huo umekuwa ukitumia wastani wa Sh35.8 bilioni kusafisha damu kupitia huduma ya dialysis.

Dialysis inavyofanya kazi

Dialysis ya figo ni matibabu ambayo kawaida hujumuisha kutumia mashine kuchukua kazi ya figo kuchuja sumu, taka na maji kupita kiasi kutoka mwilini. Tiba hii huhitajika na wagonjwa ambao figo zao hazifanyi kazi vizuri.

Mgonjwa huanza kufanyiwa tiba hiyo kwa kiwango maalumu atafanya mara tatu mpaka nne kwa siku na baadaye ataanza kufanyiwa kwa shift atapangiwa mara tatu kwa wiki.

Ndani ya mashine mgonjwa anatakiwa kukaa kwa saa nne, kwani mgonjwa akishafikia hatua ya figo kutokufanya kazi ambazo ilikuwa kutoa sumu, maji machafu, kupunguza maji mwilini, figo haiwezi kufanya kazi zake inabidi itegemee mashine ambayo hufanya kazi za figo.

Figo ikishindwa kupewa huduma hizo, mgonjwa atapoteza maisha kwakuwa atashindwa kupumua, ataongezeka uzito, maji yaliyotakiwa yatoke yote yatabaki mwilini.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live