Serikali imetaja magonjwa 10 yaliyowatikisa Watanzania mwaka 2023, maambukizi ya njia ya mkojo (UTI) na mfumo wa hewa yakiwakumba wengi.
Maambukizi ya mfumo wa hewa yaliwaathiri Watanzania 4,901,844 (sawa na asilimia 18.9), huku UTI ikiathiri watu 4,095,104 (asilimia 15.8). Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alibainisha hayo jana jijini Dar es Salaam, alipozungumza na waandishi wa habari akieleza mafanikio na mikakati ya wizara hiyo kwa mwaka 2024.
Katika orodha, Waziri Ummy alisema malaria iliathiri watu 1,772,523 (asilimia 6.9), shinikizo la damu watu 1,455,165 (asilimia 5.6) na vidonda vya tumbo watu 963,520 (asilimia 3.7).
New Content Item (1)
Mengine ni magonjwa yasiyo ya kuambukiza ambayo yaliathiri watu 830,059 (asilimia 3.2), homa ya mapafu watu 703,666 (asilimia 2.7), kisukari kiliathiri watu 652,455 (asilimia 2.5), minyoo watu 611,538 (asilimia 2.4) na magonjwa mchanganyiko ambayo yaliathiri watu 552,661 (asilimia 2.1).
Mafua, kikohozi na watoto
Kwa watoto chini ya miaka mitano, Waziri Ummy alitaja magonjwa yalioongoza kwa wagonjwa wa nje kuwa ni mafua na kikohozi vikiathiri watoto 5,410,576.
Mengine ni kuharisha bila upungufu wa maji ulioathiri watoto 1,168,763, huku malaria ikiathiri watoto 1,483,845.
Waziri alisema pia yapo maambukizi kwa njia ya mkojo (UTI) ambayo yaliwaathiri watoto 1,050,723, homa ya mapafu (1,029,548), maambukizi ya ngozi (526,983), magonjwa ya mfumo wa chakula (524,698), minyoo (402,425), kuharisha na upungufu wa maji (319,686) na maambukizi ya ngozi (308,353).
Shaka ya vipimo
Akizungumzia vipimo vya UTI vinavyotiliwa shaka usahihi wake, Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Tumaini Nagu alisema majibu ya ugonjwa huo hayapaswi kuwa ya papo kwa hapo.
Alisema ili kubaini vimelea vya ugonjwa huo, ni lazima sampuli ioteshwe kwa saa 24.
Dk Nagu aliwataka wataalamu kuhakikisha vipimo vya ugonjwa huo vinaingia maabara kufanyiwa uchunguzi wa kina ndipo wagonjwa wapewe dawa, pasipo kufanya hivyo, alisema ni kuongeza tatizo la usugu wa dawa kwa wananchi.
“Wataalamu wote wa maabara wahakikishe kimelea cha UTI wanachokibaini kinaendana na dawa inayotolewa kwa mgonjwa,” aliagiza.
Ni kwa vipi ujikinge
Akizungumzia namna ya kujikinga na maradhi hayo, Waziri Ummy aliitaka jamii kutoyapuuza mafundisho ya Profesa Mohamed Janabi, mkurugenzi mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, kuhusu ulaji unaoshauriwa kiafya.
“Watu wanafanya mzaha na Profesa Janabi na mafundisho anayotoa, japokuwa wakati mwingine hata mimi ananitisha, mimi ni mwanafunzi wake na ameniharibu tangu Mei mwaka jana sinywi chai yenye sukari," alisema.
Naye mtaalamu mshauri wa afya ya jamii, Festo Ngadaya alisema kwa magonjwa yasiyo ya kuambukiza ni muhimu jamii ikapunguza ulaji wa vyakula vya wanga kupita kiasi na kuzingatia mazoezi.
Kwa magonjwa ya mlipuko na homa ya matumbo, alisema usafi na kuepuka vyakula vibichi ni njia ya kujikinga na magonjwa hayo.
“Suala la usafi ni muhimu sana, unaweza kutoka umeshikana na watu, umepanda daladala ukifika nyumbani au unaweza kupata kitu unakula bila kunawa; hapohapo unamshika mtoto mdogo, kwa hiyo sasa hivi kutokana na Uviko-19 kupungua, watu wanachangamana, hivyo tuzingatie usafi,” alisema.
Kuhusu wajawazito
Akitoa takwimu za wajawazito waliojifungulia vituo vya afya, Waziri Ummy alisema kiashiria kikuu cha ubora wa huduma za afya katika nchi yoyote duniani ni kiwango cha wajawazito wanaojifungulia katika vituo vya kutoa huduma za afya.
“Mwaka 2023 wajawazito 2,391,427, sawa na asilimia 97.5 walihudhuria kliniki mara nne katika kipindi cha ujauzito wao, lengo la nchi ni kufikia asilimia 80 mwaka 2030 kama inavyoelekezwa na Shirika la Afya Duniani (WHO),” alisema.
Alisema mwaka 2022 waliojifungua vituo vya kutoa huduma walikuwa asilimia 81 na mwaka 2023 wakaongezeka hadi asilimia 85, wakiwa zaidi ya lengo la WHO.
Ongezeko hilo analitaja kuwa ni hatua nzuri kufikia asilimia 95 kwa nchi kuwa na wajawazito wanaojifungulia kwenye vituo vya kutolea huduma za afya ifikapo mwaka 2030.
“Mwenendo huu wa utumiaji wa huduma unaendana na takwimu zinazosema vifo vitokanavyo na uzazi vimepungua kwa asilimia 80 kutoka vifo 556 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2016 hadi 104 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2022,” alisema.
“Malengo ya dunia na ya kitaifa ni kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kufikia 70 kwa kila vizazi hai 100,000 ifikapo mwaka 2030.”
Utalii wa tiba
Katika hatua nyingine, Waziri Ummy alisema kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanyika katika kuboresha huduma za kibingwa na bobezi, Tanzania mwaka 2022 ilivutia watu 1,699 kuja kupata matibabu nchini.
"Takwimu za mwaka 2023 zinaonyesha jumla ya wagonjwa 1,937 waliotoka nje ya nchi walikuja kutibiwa nchini,” alisema. Ummy alisema wagonjwa hao walitoka mataifa ya Comoro, Malawi, Burundi, Zambia, Congo DRC, Uganda, Zimbabwe na Kenya.
Wagonjwa hao, alisema walihudumiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI), Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Taasisi ya Mifupa (MOI) pamoja na hospitali za Aga Khan na Saifee.
Changamoto sekta ya afya
Licha ya mafanikio hayo, Waziri Ummy alisema sekta ya afya inakabiliwa na upungufu wa watumishi, hasa wataalamu wa maabara, wa misuli na usingizi.
“Tuna changamoto ya ubora kwa baadhi ya maeneo ya utoaji wa huduma za afya kutokana na usimamizi usioridhisha kwa baadhi ya watumishi,” alisema.
Alisema kuna mwitikio mdogo wa wananchi kujiunga na mifuko ya bima ya afya, hivyo kushindwa kugharimia huduma wanazozihitaji. Changamoto nyingine, alisema ni kuongezeka kwa magonjwa yasiyo ya kuambukiza, akitoa mfano wa kisukari.
Pia kuna tatizo la kuibuka kwa magonjwa ya watoto yanayozuilika kwa chanjo kama vile surua, polio na tetekuwanga, hali inayosababishwa na wazazi wengi kutowapeleka watoto wao kupata chanjo kwa wakati.
“Mwaka 2023 kulitolewa taarifa ya ugonjwa wa polio kwa mtoto katika Manispaa ya Mpanda, ugonjwa ambao kwa kipindi kirefu ulikuwa umedhibitiwa nchini,” alisema.
Katika kukabiliana na changamoto hizo, Waziri Ummy alisema Serikali imeweka kipaumbele katika kuimarisha afua za kinga ili kuwawezesha wananchi kujikinga na magonjwa na utambuzi wa mapema wa maradhi hayo.
Kipaumbele kingine alisema ni kutekeleza Sheria ya Bima ya Afya kwa wote ili kuwawezesha wananchi wengi kupata huduma za afya bila kikwazo cha fedha.
“Tutaongeza idadi ya watumishi wa afya katika ngazi zote na kuwajengea uwezo watumishi walio kazini kwa kuwapeleka madaktari bingwa walioko hospitali za rufaa za mikoa katika vituo vya afya na hospitali za wilaya kutoa mafunzo kwa vitendo kuhusu utoaji wa huduma bora za afya kwa wajawazito na watoto,” alisema.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa Januari 6, alinukuliwa na gazeti hili akisema Serikali itatoa ajira mpya za walimu na maofisa afya 23,000 katika kipindi cha Januari hadi Februari, mwaka huu. Alisema hayo alipofunga kikao kazi cha makatibu tawala wasaidizi elimu na maofisa elimu wa halmashauri kilichofanyika mkoani Morogoro.
Waziri Ummy alisema maeneo mengine ni kuongeza uwezo wa ndani wa kuzalisha vifaa, vifaatiba na dawa, kukamilisha mwongozo wa gharama wa utoaji huduma za afya kwenye vituo vya kutolea huduma za afya za umma ili kuwa na uwiano sawa wa bei za utoaji wa huduma.
Kukomesha wizi wa dawa
Mfamasia Mkuu wa Serikali, Daudi Msasi, alizungumzia tatizo hilo akisema dawa zote zinazotolewa na Serikali zina nembo maalumu na endapo kuna uchepushaji, Mamlaka ya Dawa na Vifaatiba (TMDA) inafanya ukaguzi wa mara kwa mara na kubaini uhalifu huo.