Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Madudu yabainika mfuko wa NHIF Mbeya, Moshi

Ummy NHIF Madudu yabainika mfuko wa NHIF Mbeya, Moshi

Tue, 6 Sep 2022 Chanzo: Mwananchi

Wakati Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu akiupa siku 14 Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kumpelekea mikakati ya kudhibiti udanganyifu unaofanywa kwa kutumia mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), naibu waziri wake, Dk Godwin Mollel amebaini ubadhirifu mkoani Mbeya na wilayani Moshi mkoani Kilimajaro.

“Kuna polyclinic Mbeya ambayo imefanya ubadhilifu wa fedha za NHIF na wahusika walitoroka nyumba waliyokuwa wakiitumia, Moshi hatua zimeshachuliwa na wahusika wanarejesha hizo fedha,” alisema Dk Mollel.

Dk Mollel jana alisema waziri wa Afya anapambana na vitu vinavyotaka kuiua NHIF. Alisema lengo ni kuonyesha kuwa na mfuko wa bima ya afya kwa wote inakuwa na uwezo mkubwa wa kuwahudumia wananchi.

Akiwa na Kamati ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii hivi karibuni jijini Dar es Salaam, Dk Mollel alisema, wataalamu walioagizwa kufanya uchunguzi wamebaini ubadhilifu wa Sh1.6 bilioni za NHIF Mbeya mjini pekee.

Polyclinic aliyoitaja Dk Mollel alisema imetoweka na Sh137 milioni za NHIF ambayo waliibaini kutoa huduma kwenye nyumba ya wageni na walipoifuatilia ili kuwakamata wahusika walikuta wametoweka kusikojulikana.

Alibainisha mbinu zilizotumika kuchota fedha hizo ni utengenezaji wa fomu 2C na kuwaandikia watu huduma ambazo hawakuzitumia pamoja na kuzitumia vibaya kadi za NHIF.

Kuhusu Moshi mkoani Kilimanjaro alisema walibaini kituo kimoja cha afya kufanya ubadhilifu wa Sh520.

NHIF yanena

Ofisa Uhusiano wa NHIF, Grace Michael alisema wanapambana na udanganyifu wa njia mbalimbali ikiwamo kuwachunguza kwa kina watoa huduma, waajiri, wanachama, watumishi wa mfuko na watu wanaoweza kushiriki kuuhujumu.

“Katika mwaka wa fedha 2021/22, mfuko umefanya zaidi ya uchunguzi 86 na kufanikiwa kurejesha zaidi ya Sh7.9 bilioni...pamoja na wahusika kurejesha fedha zilizolipwa kwa udanganyifu,” alisema Grace.

Baada ya uchunguzi huo, Grace alisema NHIF imewamuru wahusika kuzirejesha fedha zililipwa kwa udanganyifu, wanataaluma 65 kwa mwaka waliohusika wameripotiwa katika mabaraza yao ya taaluma kwa ajili ya hatua zaidi.

Kwa wanachama 141 waliohusika na udanganyifu na vituo 14 alisema vilisitishiwa mikataba yao.

Kwa fedha zilizoibwa Kilimanjaro, Grace alisema hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kuzirejesha Sh520.1 milioni na wahusika kuripotiwa Takukuru wakati wataalam wakifikishwa katika mabaraza yao. Kilichofanyika mkoani Mbeya alisema polyclinic inaitwa St. Elizabeth imefungiwa.

“Jumla ya Sh984 milioni zimerejeshwa Mbeya, mfuko unaendelea kuimarisha mifumo yake ili kuzuia udanganyifu na kugundua viashiria vya udanganyifu mapema,” alisema Grace.

Chanzo: Mwananchi