Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Madhara ya kuzaa bonge, wataalamu waonya

Mtoto Mtoto.jpeg Madhara ya kuzaa bonge, wataalamu waonya

Tue, 12 Dec 2023 Chanzo: mwanachidigital

Kama unafurahia kupata mtoto mwenye uzito kupita kiasi unapaswa kutafakari upya na uchukue hatua kwa kuwa huenda unafurahia maisha ya mwanao kuwa hatarini.

Hiyo ni kwa mujibu wa wataalam wa afya ambao wanaungwa mkono na akiwemo Profesa Mohamed Janabi kuwa mtoto kuzaliwa akiwa na uzito wa zaidi ya kilo nne ni kiashiria cha magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

Tovuti ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) katika makala yake kuhusu watoto wenye uzito kupita kiasi, inaeleza kuwa asilimia 12 ya watoto wa aina hiyo, huzaliwa kwa wanawake wanaokuwa na ugonjwa wa kisukari wakati wa ujauzito.

Kujifungua mtoto mwenye uzito mkubwa mara nyingi huambatana na madhara mbalimbali kwa mama na mtoto, kama vile kifo cha kichanga na mama au kuongeza hatari ya kupata ugonjwa wa kisukari aina ya 2, magonjwa ya moyo na saratani kwa watoto hao katika siku za usoni.

Kulingana na wataalamu, kwa kawaida wastani wa uzito wa mtoto unapaswa kuwa kilo 3.3 kwa mtoto wa kike na 3.2 kwa mtoto wa kiume.

Mbali na maradhi hayo, watoto wenye uzito mkubwa wana uwezekano mkubwa wa kupata ugumu wa kuzaliwa kupitia njia ya kawaida kutokana na ukubwa wao hivyo kusababisha mzazi ama afanyiwe upasuaji au aongezwe njia.

Taarifa za kitaalamu zinaonyesha wanawake wanaojifungua watoto wenye uzito mkubwa wapo katika hatari ya kuchanika uke wakati wa kujifungua, jambo ambalo huongeza hatari ya kuvuja damu baada ya kujifungua.

Pia, mama anapokuwa mnene zaidi wakati wa ujauzito kutokana na ulaji wa mara kwa mara, hususan ulaji wa wanga kwa wingi, mafuta na mayai pamoja na chips, hatari yake ni uwezekano wa kujifungua mtoto mnene kupita kiasi.

Profesa Janabi, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), aligusia suala hilo juzi usiku wakati wa hafla uzinduzi wa Taasisi ya Profesa Jay jijini Dar es Salaam, yenye lengo la kuchangia fedha za matibabu ya wagonjwa wa figo.

Taasisi hiyo imeanzishwa na Mbunge wa zamani wa Mikumi (Chadema) na msanii wa Hip Hop, Joseph Haule maarufu Profesa Jaybaada ya kuugua ugonjwa wa figo uliomfanya kulazwa hospitalini siku 462, matibabu aliyosema yalikuwa ya gharama kubwa.

Katika maelezo yake, Profesa Janabi alisema ugonjwa figo ambao Profesa Jay anapambana nao chanzo chake kikubwa ni ugonjwa wa kisukari ambao unaendana na mfumo mbovu wa maisha.

Akifafanua, alisema huo mfumo wa maisha unaoleta madhara hadi kuambukiza mtoto aliyeko tumboni.

Alitolea mfano, kuwa mama mwenye kisukari ni rahisi kuzaa mtoto mwenye uzito kupita kiasi kwa kutokana na ile sukari inayozalishwa kwenye damu kumfikia.

“Mtoto aliyezaliwa na uzito mkubwa yuko hatarini kupata magonjwa yasiyo ya kuambukiza na jamii haipaswi kufurahi mama anapojifungua mtoto mwenye uzito mkubwa kwa kuwa ni hatari kiafya.

"Pale wodi ya wazazi unaona mtu amejifungua mtoto mwenye kilogramu nne, ndugu wanasema mashallah, hapo hamna mashallah mtoto ni over weight (amezidi uzito), si jambo kufurahia ni tatizo,” alisema.

Profesa janabi alisema “si sahihi kwa mtoto kuzaliwa akiwa na uzito mkubwa kupita kiasi, tujitahidi kupunguza uzito.”

Alisema ukiwa mzazi mnene hali hiyo unaiambukiza kwa mtoto.

“Sasa hivi tunashuhudia watoto wadogo wanakuja Muhimbili figo zimeharibika tunalazimika kuwapandikiza,” alisema Profesa Janabi.

Mariana Luvanga, mama mwenye watoto watatu alisema mara zote anapokuwa mjamzito hujitahidi kuzingatia maelekezo anayopewa kliniki na hajawahi kukutana na changamoto ya kupata mtoto mwenye uzito mkubwa au mdogo kupita kiasi.

“Ninachofahamu msisitizo mkubwa kwa mama mjamzito ni kula lishe bora ili kutoa virutubisho muhimu kwa mtoto anayekua tumboni. Hii ni pamoja na kula matunda, mboga, nafaka nzima, nyama, samaki, maziwa na bidhaa za maziwa.

“Kingine ni mazoezi mepesi ambayo ni msaada kwa mama hata kuufanya mwili wake usichoke na kumuondolea uwezekano wa kujifungua kwa upasuaji. Binafsi sijawahi kukutana na changamoto kubwa zaidi ya zile za kawaida za miezi mitatu ya mwanzo,” alisema Mariana

Wakati Mariana akieleza hayo, mmoja wa wazazi ambaye amewahi kupata mtoto mwenye uzito mkubwa aliliambia gazeti hili kwa miaka 11 mtoto wake ameendelea kuongezeka uzito, hali inayomfanya kuwa mvivu.

“Mtoto wangu alizaliwa na kilo 5.8 na alizaliwa kwa upasuaji, hadi sasa hatujagundua ugonjwa wowote ila naweza kusema mwili wake unamfanya kuwa mvivu. Sio mtu wa kujichanganya na licha ya kufanya mazoezi kidogo lakini uzito wake unaendelea kuongezeka,” alisema mzazi huyo ambaye hakutaka jina lake liwekwe wazi.

Gazeti hili lilizungumza na mkunga mstaafu, Salome Milinga aliyesema yapo mambo yanayochangia mjamzito kujifungua mtoto mwenye uzito kupita kiasi, ikiwemo mama kuwa na asili ya uzito mkubwa kabla ya ujauzito, kuongezeka uzito kupita kiasi wakati wa ujauzito na mama kuzaliwa na uzito mkubwa.

“Uzito wa mama unachangia kwenye uzito wa mtoto atakayezaliwa, ndiyo maana wakati wote kliniki huwa tunawasisitiza wazingatie mlo kamili, wasiache kula kwa sababu ni kipindi ambacho mwili unahitaji chakula lakini lazima iwe ni kiasi, si kutwa vyakula vya wanga na mafuta.

Sababu nyingine, anasema hutokea kwa akina mama wenye kisukari kwa sababu kwenye damu ya mama, hapa upo uwezekano wa mtoto kuzaliwa na uzito mkubwa kwa sababu anapata glucose nyingi mno kutoka kwenye damu,” alisema mkunga huyo.

Profesa Jay na shukurani

Akizungumza kwenye halfa hiyo, Mwenyekiti wa Profesa Jay Foundation, Joseph Haule alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa namna alivyoelekeza Serikali igharamie matibabu yake ndani na nje ya nchi pamoja na mchango wake wa Sh50 milioni kwa ajili ya taasisi hiyo.

Profesa Jay ambaye alikuwa mgonjwa kwa zaidi ya mwaka mmoja akisumbuliwa na maradhi ya figo, aliingia ukumbini hapo akiwa kwenye kiti cha magurudumu akiambatana na wageni wengine katika hafla ya uzinduzi huo ulioambatana na harambee ya kutunisha mfuko wa matibabu ya magonjwa ya figo.

Miongoni mwa waliohudhuria na kuchangia hafla hiyo ni Makamu Mwenyekiti wa Chadema-Bara, Tundu Lissu (Sh2 milioni), Katibu wa Chadema, John Mnyika 9Sh2 milioni), Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Gobless Lema (Sh3 milioni), John Heche (Sh1 milioni na marafiki wa Chadema Sh3 milioni).

Wengine ni wasanii akiwemo, Lady Jaydee (Sh2 milioni) Gabo na wasanii wenzake wa filamu Sh3 mililioni), Chege na Temba (Sh2 milioni) Alikiba na King Music Sh5 milioni pamoja na Weusi Sh1 milioni.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alitoa Sh10 milioni, Timu ya Yanga ilitoa Sh5 milioni huku wanasiasa wengine wakiotoa michango mbalimbali kabla ya taasisi hiyo kuzinduliwa.

Chanzo: mwanachidigital