Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa mara nyingine imeandika historia kwa kufanya upasuaji mkubwa wa kuwatengenisha watoto mapacha waliokuwa wameungana sehemu ya tumbo na kifua na kuwa upasuaji wa kwanza kufanywa na madaktari wazawa hapa nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji Dkt. Rachel Mhaville amesema upasuaji huo umefanikiwa kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita kwa kununua vifaa tiba vya kisasa pamoja na kuwasomesha wataalamu.
“Tunachojivunia katika upasuaji huu ni kuwa umefanywa na timu ya madaktari wazawa, umefanyika kwa mafaniko makubwa na watoto wanaendelea vizuri kabisa. Lakini pamoja na kufanikiwa kufanya upasuaji huu bado tutaendelea kushirikiana na wataalamu wengine kwa ajili ya kuendelea kupata ujuzi zaidi na kuendeleza uhusiano” amesisitiza Dkt. Mhavile.
Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Watoto Hospitali ya Taifa Muhimbili Dkt. Victor Ngota ameeleza kuwa upasuaji wa kuwatenganisha watoto unahitaji utaalamu wa hali ya juu hivyo ulihusisha jopo la wataalamu mbalimbali ikiwemo madaktari bingwa ikiwemo wa upasuaji watoto, upasuaji rekebishi, wataalamu wa usingizi ,wataalamu wa lishe pamoja na wataalamu wa radiolojia.
“ Tuliwapokea watoto hawa tarehe 11 Machi 2023 hivyo tulianza mchakato wa kuwahusisha wataalamu ambao wanahusika na huduma hizi, ilituchukua takribani muda wa miezi kumi kuangalia mwenendo wao wa afya kwa ujumla kabla ya kuwatenganisha ili kuweza kupata dira ya namna watakavyoishi mara baada ya kutenganishwa” amefafanua Dkt. Ngota.
Upasuaji huo umefanyika kwa muda wa takribani saa sita hadi kukamilika ambapo ni wa kwanza kufanywa na mdaktari wazawa hapa nchini na kuwa upasuaji wa nne kufanyika katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.