Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Madaktari wataja mbinu kukabili athari za joto

30045 Pic+joto Madaktari wataja mbinu kukabili athari za joto

Wed, 10 Nov 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MADAKTARI bingwa wametaja mbinu ambazo Watanzania wanatakiwa kuchukua kukabili ongezeko la joto ikiwemo kunywa maji mengi, kuepuka msongamano na kuepuka kukaa juani.

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa taarifa ikieleza kuwepo ongezeko la joto maeneo mengi nchini.

Daktari bingwa wa upasuaji ubongo, uti wa mgongo na mishipa ya fahamu kutoka Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), Dk Laurent Mchome alisema ongezeko la joto lina madhara kiafya katika mwili wa binadamu.

Alisema kutokana na mabadiliko ya tabia nchi kwa sasa miale ya jua ikimpiga mtu mwilini inaathiri moja kwa moja ngozi na hivyo kuwa na uwezekano mkubwa wa kupata saratani ya ngozi.

“Lakini pia madhara mengine ya kiafya kwa binadamu kutokana na joto ni ugonjwa wa Heart Stroke unaotokana na mwili kupata joto sana kiasi cha maji kukauka hali inayosababisha kifo,” alisema Dk Mchome.

Alitaja mbinu za kuepuka madhara ya joto kuwa ni kunywa maji mengi angalau lita mbili hadi tatu kwa siku hususani kwa wanaofanyakazi ngumu zinazowatoa jasho jingi, kuepuka kukaa juani bila sababu na kuyakinga makundi ya watu walio hatarini kama vile watoto na wazee.

“Kwa watoto hususani wale wa siku sifuri hadi mwezi mmoja ni hatari zaidi katika kukabiliana na joto kwani bado kinga yao iko chini,” alieleza.

Pia alishauri katika kipindi hiki cha joto, ni vyema usafiri wa umma ukaepuka msongamano na kujaza abiria kupita kiasi na madirisha kufunguliwa ili hewa safi iingie ndani.

“Hebu fikiria na joto hili, nje jua kali halafu daladala imejaza kupita kiasi, hali hii ni hatari sana hasa kwa watoto, wazee na hata wagonjwa,” alieleza.

Daktari Bingwa wa Huduma za Dharura, Dk Deus Kitapondya alisema hali ya sasa ya joto ina mabadiliko makubwa kwani kuna maeneo yaliyozoeleka kuwa na hali ya hewa ya wastani kama vile Tabora, Shinyanga na Kilimanjaro, lakini sasa joto limeongezeka kwenye maeneo hayo.

Alisema ingawa bado Tanzania haijafikia kiasi cha kuwa na joto la kutisha kama ilivyo kwa nchi kama India na Pakistan, lakini kutokana na ongezeko la joto kupanda kila mwaka, kuna haja ya kuchukua tahadhari za kiafya.

“Joto linaweza kusababisha magonjwa kama vile Heart Stroke, lakini pia huathiri utendaji wa mwili kiasi cha kuhitaji matumizi ya feni, kiyoyozi na kunywa maji mengi,” alieleza Dk Kitapondya.

Alisema hadi mwili wa binadamu uanze kuathirika na joto na kusababisha kifo au magonjwa ni likifikia nyuzi joto 41 kwa kuwa hukausha maji mwilini na wakati mwingine husababisha presha kushuka na mwili kushindwa kufanyakazi.

Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu wa Shughuli za Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali Jimmy Matamwe alisema kwa kuwa maafa ni suala mtambuka, idara hiyo imekuwa ikishirikiana na taasisi mbalimbali kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna ya kuchukua tahadhari.

Alisema TMA ni mdau wa idara hiyo na kwamba taarifa yake ya ongezeko la joto, idara hiyo imeichukua na kuichakata kwa ajili ya kutafuta watalaamu watakaoelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kuchukua tahadhari.

Katika taarifa yao, TMA ilieleza kuwa katika kipindi hiki viwango vya joto vilivyoripotiwa katika maeneo mbalimbali ni vikubwa ambapo Mkoa wa Kilimanjaro uliripoti kiwango cha juu cha joto kilichofikia nyuzi joto 36.4 sawa na ongezeko la nyuzi joto 4.6 ukilinganisha na wastani wa muda mrefu kwa mwezi Novemba.

Vilevile, kiwango cha juu cha joto katika Mkoa wa Dar es Salaam kimefikia nyuzi joto 33.8 sawa na ongezeko la nyuzi joto 2.2 wakati katika Mkoa wa Ruvuma kimefikia nyuzi joto 34.4 sawa na ongezeko la nyuzi joto 4.3.

Chanzo: www.habarileo.co.tz