Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Madaktari washauriwa kuwapeleka wagonjwa JKCI mapema

12506 MOYO+PIC TanzaniaWeb

Fri, 17 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Madaktari wa Hospitali za Rufaa nchini wameshauriwa  kuwapeleka  mapema wagonjwa wa moyo katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) pindi wanapopimwa na kugundulika  kuwa na ugonjwa   huo ili wapate tiba mapema.

Rai hiyo imetolewa leo Agosti 17 na Mkurugenzi wa Tiba Shirikishi ambaye pia ni Daktari bingwa wa magonjwa ya Moyo  kutoka JKCI Delila Kimambo wakati wa mkutano wa kwanza wa kitaifa wa kutathmini magonjwa ya moyo nchini uliofanyika   katika ukumbi wa mikutano wa  Taasisi hiyo.

Dk Delila amesema wagonjwa wa moyo wanaotibiwa katika Hospitali mbalimbali hapa nchini rufaa yao huwa ni Taasisi ya Moyo hivyo basi ni muhimu wagonjwa hao wakafika katika Hospitali hiyo kwa wakati.

“Wagonjwa wengi tunaowapokea mioyo yao huwa imechoka, kama wagonjwa hawa wangefika  mapema kwetu wangepata matibabu madogo  kuliko kupatiwa matibabu makubwa ya upasuaji wa kifua au bila kufungua kifua kwa kutumia tundu dogo”.

“Kutokana na wagonjwa wengi kuchelewa kufika hospitalini ama kutokupata matibabu ya moyo kwa wakati, tumeona tuwe na mafunzo haya hii itawasaidia madaktari wengi kupata ujuzi zaidi  na kuweza kutambua wagonjwa kwa wakati”, amesema Dkt. Delila.

Akizungumzia kuhusu mkutano huo Dkt. Delila mesema lengo ni kuwapatia madaktari ujuzi hususani wa namna ya kupima moyo kwa kutumia mashine za ECHO na umeme wa moyo (Electrocardiography – ECG).

Kwa upande wake Daktari kutoka hospitali ya Amana Natalius Kapilima alisema mafunzo hayo yamewasaidia kupata ujuzi utakaowawezesha kuwatambua wagonjwa wa moyo kupitia vipimo vya Echo na ECG.

Kwa upande wake, Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka hospitali ya Aga Khan Profesa Mustafa Bapuma ameishukuru Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete kwa kuona mbali na kuwezesha  kufanyika kwa mafunzo hayo kwa madaktari. Kupitia mafunzo hayo wataweza kutibu wagonjwa wa moyo kwa ustadi na ufanisi zaidi kuliko hapo awali.

Mkutano huo wa siku moja umeandaliwa na  Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete kwa kushirikiana na Kampuni ya Merck ambapo jumla ya washiriki 80 kutoka Hospitali mbalimbali za mkoa wa Dar es Salaam walishiriki.

Chanzo: mwananchi.co.tz