Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Madaktari waonya, waeleza madhara ya kulala na simu

86137 Pic+simu Madaktari waonya, waeleza madhara ya kulala na simu

Thu, 28 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Madaktari bingwa wa ubongo na mishipa ya fahamu na wale wa magonjwa ya saratani wanaonya kuwa kulala karibu na simu kuna madhara kiafya na kunaweza kusababisha mtu kupata saratani.

Daktari bingwa wa upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu wa Hospitali ya Aga Khan, Dk Mugisha Clement alisema kwamba kulala na simu karibu kuna madhara kiafya.

Akifafanua Dk Clement alisema simu hutoa mionzi ambayo inaweza kusababisha saratani, ingawa alibainisha kwamba jambo hilo bado limewagawanywa watafiti ingawa Shirika la Afya Duniani WHO nalo limeshawaonya watu dhidi ya madhara hayo ambayo bado yanachunguzwa.

“Utafiti umefanywa lakini wanasayansi bado hawajapata ushahidi wa kutosha ya kuwa mionzi (radiofrequency field) inayotolewa na simu haikuwa/haina athari yoyote kwenye ubongo au mshipa ya fahamu,” alisema Dk Mugisha.

Naye daktari kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila, Dk Patrick Kushoka alisema kwamba simu za mkononi zimechangia ongezeko la magonjwa hasa ya saratani ya ubongo.

“Kutokana na ongezeko la matumizi ya simu za mkononi na vifaa vingine vya kielektroniki, tafiti zinaonyesha kuwapo ongezeko la magonjwa hasa ya saratani ya ubongo,” alisema.

Dk Kushoka alisema licha ya saratani, tafiti pia zinaonyesha kupungua kwa uwezo wa ubongo kufanya kazi yake vyema ikiwemo usahaulifu, hii ni kutokana na mionzi inayozalishwa (electromagnetic fields) na vifaa hivyo ikiwemo simu za mkononi.

“Katika utafiti wa ‘INTER-PHONE International case-control study’ uliofanyika kwenye nchi kadhaa zikiwemo za Australia, Denmark, Finland, Ufaransa, Israel, Japan, Canada, Ujerumani, Norway, New Zealand, Uswisi na Italia, umeonyesha ongezeko la magonjwa haya ni kubwa zaidi kwa watu wanaotumia vifaa hivi kuanzia miaka 10 ya matumizi na kuendelea,” alisema Dk Kushoka.

Kwa upande wake mtaalamu wa magonjwa ya saratani kutoka Hospitali ya Ocean Road, Dk Maghuha Stephano alisema kwamba mionzi yoyote inapompiga mtu kwa muda mrefu husababisha saratani.

“Japokuwa tafiti bado zinaendelea kuleta majibu haya lakini ni lazima tutambue kuwa mionzi inahusishwa na saratani kwa kiasi kikubwa lakini hii iliyopo kwenye simu isipuuzwe.”

Kwanini simu ya mkononi ina madhara?

Simu imetengenezwa katika njia ambayo inahusika moja kwa moja kutoa mionzi kwa lengo la kufanikisha mawasiliano, mionzi hiyo hatari inafahamika kama electromagnetic radiation ambayo hutokana na x-ray & microwaves.

Mionzi hii ni hatari kiafya kwani ina nguvu kiasi cha kuweza kupenya kwenye ngozi mpaka kwenye fuvu la kichwa jambo ambalo huathiri mfumo wa fahamu na kusababisha uvimbe kwenye ubongo kisha huzaa saratani ya ubongo.

Tahadhari

Epuka kulala karibu na simu yako au kuweka chini ya mto wakati wa kulala na kama ni lazima kufanya hivyo hakikisha walau simu hiyo iwe mita moja na nusu kutoka mahali ulipolala na endapo unaona ni vigumu basi ni vizuri ukaizima.

Unapopiga au kupigiwa simu ni vizuri kutumia earphone ili kuepuka kuweka simu karibu na kichwa, endapo huna earphone basi usitumie sikio moja kusikiliza simu uwe unabadilisha.

Usiwape watoto wachanga simu kwani wao huathirika kirahisi sana na mionzi kwa kuwa fuvu lake ni jepesi na hivyo mionzi hupenya kirahisi.

Unapotumia simu nyakati za usiku ni vizuri ukapunguza kiasi cha mwanga (brightness) ili kujilinda na madhara ya miale ya bluu.

Chanzo: mwananchi.co.tz