Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Madaktari waipa kongole Serikali kuwasikiliza

Tue, 5 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Chama cha Madaktari Tanzania (Mat) kimesema Serikali imeleta maendeleo makubwa katika sekta ya afya kwa kusikiliza na kutekeleza mapendekezo yao, hivyo ushirikiano huo ukiendelea nchi itafika katika viwango vya juu katika utoaji wa huduma za afya.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa maadhimisho ya Siku ya Taifa ya Madaktari nchini, Rais wa Mat, Dk Elisha Osati alisema kwa sasa hali ya huduma za afya nchini ni nzuri kulinganisha na nyuma.

“Tunashukuru Serikali licha ya kukubaliana na mawazo yetu, maendeleo yote tunayoshuhudia kwa sasa ni mawazo ya madaktari kama wanataaluma na Serikali inayabariki,” alisema Dk Osati.

Alisema kwa sasa hali ya huduma ni nzuri kulinganisha na miaka michache nyuma.

Dk Osati aliyataja maendeleo ambayo Tanzania imepiga katika huduma za afya kuwa ni upasuaji moyo, kupandikiza figo, masikio kwa watoto wadogo na mafunzo yanayoendelea katika kupandikiza ini na mifupa.

Pamoja na hayo, Dk Osati alisema changamoto ambazo Serikali inapaswa kuwekeza zaidi ni eneo la rasilimali watu.

Alisema kwa viwango vya Shirika la Afya Duniani (WHO) daktari mmoja anatakiwa kuhudumia wagonjwa chini ya 10,000 kwa mwaka lakini kwa sasa daktari mmoja anahudumia wagonjwa 20,000 mpaka 26,000 ingawa kuna sehemu mjini wanahudumia wagonjwa hadi 18,000.

Awali, mganga mkuu wa Serikali Profesa Mohamed Bakari, aliwataka madaktari kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia weledi na maadili.

Profesa Bakari ambaye alimwakilisha Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, alisema Serikali inawaunga mkono Mat katika kuleta mabadiliko katika sekta ya afya.

Naye mkurugenzi wa rasilimali watu na utawala wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) Makwaia Makani, aliwataka madaktari kuendelea kutoa ushauri katika sekta ya afya kama wanataaluma kwenye ngazi ya taifa na taasisi zao wanakofanyia kazi.



Chanzo: mwananchi.co.tz