Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Madaktari waasa usafishaji masikio kwa pamba, karatasi

C48741243f6cf4092f2bde683b706238.jpeg Madaktari waasa usafishaji masikio kwa pamba, karatasi

Sat, 6 Nov 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WATAALAMU wa afya wameonya juu ya matumizi ya vifaa visivyo rasmi kusafishia masikio wakisema ni mojawapo ya sababu za kupunguza uwezo wa kusikia.

Wakizungumza kwenye maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Hospitali ya Kanda ya Rufaa Bugando, baadhi ya madaktari kutoka Kitengo cha Masikio, Pua na Koo (ENT), walitaja vitu hatari ambavyo baadhi ya watu wamekuwa wakitumia kusafishia masikio ni funguo za gari, vipande vya karatasi pamoja na pamba.

“Tunaendelea kutoa elimu kwa jamii ili watu wote wawe na uelewa wa njia sahihi ya kulinda sikio, kufanya uchunguzi mara kwa mara pamoja na kushauri matibabu ya mapema kwa wanaogundulika na matatizo,” Bingwa wa Upasuaji, Dk Fidelis Mbunda alilieleza gazeti hili jana.

Alisisitiza kwamba mgonjwa akichelewa kupata matibabu anakuwa kwenye hatari kubwa ya kupoteza uwezo wa kusikia kwani seli za sikio zikishakufa haziwezi kufufuliwa tofauti na seli zingine katika mwili wa binadamu ambazo hutengenezwa na mwili wenyewe.

Ilielezwa sababu nyingine za kupoteza usikivu ni kukaa kwenye kelele muda mrefu, kuweka sauti kubwa ya muziki masikioni pamoja na ajali ya sikio.

Mkuu wa Kitengo cha ENT, Dk Gustave Buname alisema Bugando hupokea wagonjwa zaidi ya 2,500 kwa mwezi na asilimia 40 wana tatizo la kupoteza usikivu.

Alisisitiza kwamba chanzo ni maambukizi yanayotokana na sababu mbalimbali ikiwemo kuondolewa kwa nta ndani ya sikio bila kutumia njia sahihi pamoja na kelele za aina mbalimbali.

Alishauri kutoingiza kitu chochote ndani ya sikio bali kidole pekee linapowasha. Kwa mujibu wa Dk Buname, watu wazima wamekuwa wakisumbuliwa hususani na kuota nyama za puani, mafindofindo na kizunguzungu.

“Watoto nao wanasumbuliwa na matatizo kadhaa ya masikio na siku za nyuma haikuruhusiwa kufanyiwa upasuaji wowote kutokana na uhaba wa vifaa lakini sasa tuna mashine maalumu kwa ajili yao,” alisema.

Mmoja wa wagonjwa wa matatizo ya usikivu, Restuta Charles aliipongeza Hospitali ya Bugando kwa kutoa huduma bure za matibabu na ushauri katika maadhimisho hayo ambayo kilele chake ni Novemba 18, mwaka huu.

Aliiomba Bugando na serikali kwa ujumla kuendeleza na kudumisha huduma kama hizo za nje ya eneo la hospitali ziwafikie wananchi wengi.

Chanzo: www.habarileo.co.tz