Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Madaktari hospitali ya Aga Khan wataja takwimu ugonjwa wa kisukari

84589 Pic+kisukari Madaktari hospitali ya Aga Khan wataja takwimu ugonjwa wa kisukari

Mon, 18 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakati asilimia 9.1 ya Watanzania wanaugua kisukari, imeelezwa asilimia 71 ya wanaougua ugonjwa huo duniani wanaishi katika nchi zenye kipato cha chini.

Hayo yamesemwa leo Jumamosi Novemba 16, 2019 na mkurugenzi wa tiba wa Hospitali ya Aga Khan, Dk Ahmed Jusabani katika maadhimisho ya siku ya kisukari duniani ambayo hufanyika Novemba 14 kila mwaka.

Amesema kisukari ni janga la kimataifa na kwamba takwimu zinaonyesha wanaougua kwa sasa ni chini ya miaka 65 ikilinganisha na zamani ilikuwa zaidi ya umri huo.

“Asilimia 80 ya watu wanaoishi na ugonjwa huu wapo chini ya miaka 65 na vijana ndiyo wanaathirika ikilinganishwa na zamani, watoto zaidi ya milioni moja wanaishi na ugonjwa huu na asilimia 71 ya wagonjwa ni wale wanaoishi katika nchi zenye kipato cha chini au cha kati,” amesema.

Dk Jusabani amesema hospitali ya Aga Khan inatoa  huduma hiyo kwa wagonjwa ili kubaini athari za magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo kisukari.

Daktari bingwa wa magonjwa ya ndani wa hospitali hiyo, Samina Somji amesema kila mwaka kunakuwa na mbinu tofauti kupambana na ugonjwa wa kisukari na mwaka huu kaulimbiu ni Kisukari na familia.

Amesema takwimu za sasa kiwango cha kisukari duniani ni asilimia tisa na kwa Tanzania ni asilimia 9.1, kwamba katika kila watu 10 mmoja ana kisukari.

Dk Somji amesema asilimia 50 ya wagonjwa wanaougua figo pia wana kisukari, akibainisha kuwa ugonjwa huo ni hatari kwa kuzalisha magonjwa mengine katika mwili.

Chanzo: mwananchi.co.tz