Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Madaktari bingwa wa JKCI kuweka kambi Kilimanjaro

Doctors Vichomi Madaktari bingwa wa JKCI kuweka kambi Kilimanjaro

Tue, 15 Aug 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Madaktari Bingwa wa Moyo, kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) wanatarajiwa kuweka kambi ya siku tano katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro Mawenzi, kwa ajili ya kutoa huduma za uchunguzi wa magonjwa ya moyo.

Madaktari hao bobezi wa moyo kwa kushirikiana na madaktari bingwa wa Mawenzi, watatoa huduma hiyo kuanzia Agosti 21 hadi 25 mwaka huu, lengo likiwa ni kuwapunguzia wananchi gharama za kusafiri hadi jijini Dar es Salaam, kufuata huduma hizo.

Akizungumzia ujio wa madaktari hao, leo Jumatatu Agosti 14, 2023, Mratibu wa huduma za tiba za Hospitali ya Mawenzi ambaye pia ni daktari bingwa wa watoto, Dk Michael Irira amesema, ujio wa madaktari hao wa moyo, utatoa fursa kwa wagonjwa wa moyo, kupata huduma za kibingwa kwa karibu.

Dk Irira amesema wananchi wote wenye matatizo ya moyo watakaofika Mawenzi ndani ya siku hizo tano, watahudumiwa kwa kufuata taratibu za hospitali, ambapo amewataka wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro, kuchangamkia fursa hiyo ili kuokoa gharama za kufuata huduma JKCI.

"Wagonjwa watakaohudumiwa na madaktari hao, ni wale wenye matatizo ya Moyo, ambapo uchunguzi utafanyika na wagonjwa watatoa malipo kulingana na taratibu za malipo za kawaida za hospitali hii ya Mawenzi na endapo watafanya uchunguzi na kuona kuna uhitaji wa mgonjwa kufanyiwa upasuaji, mgonjwa atapewa maelezo ya nini cha kufanya ili kupata huduma hiyo," amesema Dk Irira.

Ameongeza kuwa, "Tunajua taasisi hii iko jijini Dar es Salaam, hivyo mgonjwa kutoka hapa hadi huko ni gharama kubwa, hivyo madaktari hao kufika hapa itawawezesha wananchi kupata huduma karibu na kupunguza gharama, lakini pia hii ina lengo la kujengeana uwezo kwenye eneo hili."

Akizungumza kuhusiana na huduma hizo, Debora Maro ambaye ni mkazi wa Moshi mjini, amesema ujio wa madaktari hao utakuwa ni faraja kubwa kwa wananchi kwa kuwa wamekuwa wakitumia gharama kubwa kusafiri hadi Dar es Salaam kwa ajili ya kufuata huduma.

"Tunashukuru sana kwa taarifa za ujio wa madaktari bingwa wa Moyo hapa Mawenzi, kwani tumekuwa tukitumia gharama kubwa kwa ajili ya usafiri na malazi Dar es Salaam, lakini tunaomba isiwe mwisho, utaratibu huu uwe ni wa mara kwa mara ili kurahisishia wananchi kupata huduma za matibabu ya moyo.

Gema Kimath amesema mbali ya kupunguziwa gharama pia itawaokolea muda ambao wamekuwa wakiutumia kusafiri na kukaa Dar es Salaam kusubiria huduma na sasa watapata huduma karibu na kwenda kuendelea na majukumu yao ya kujitafutia kipato.

"Nishauri wananchi wenzangu wajitokeze kupata huduma za vipimo na uchunguzi wa moyo, ili kujitambua na kuchukua hatua za matibabu kwa wale watakaobainika kuwa na matatizo ya moyo," amesema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live