Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Madaktari bingwa 11 wa China wawasili kufanya kazi Tanzania

China Pic Data Madaktari bingwa 11 wa China wawasili kufanya kazi Tanzania

Tue, 25 Jan 2022 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Timu ya madaktari bingwa 11 kutoka Serikali ya watu wa China imewasili nchini ambapo inatarajiwa kutoa huduma za matibabu ya kibingwa kwa hospitali kuu nne nchini ikiwemo Taasisi ya tiba ya mifupa Muhimbili (MOI) kwa miaka miwili.

Pamoja na MOI taasisi zingine ambazo mabingwa hao watatoa huduma ni pamoja na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) na hospitali ya rufaa ya Kanda Mbeya (MZRH).

Madkatari hao wamewasili nchini kufuatia mkataba namba 26 ambao Septemba 2021 Serikali kupitia Wizara ya Afya iliingia mkataba wa ushirikiano na Serikali ya Jamhuri ya watu wa China.

Mkataba huo pamoja na mambo mengine ulijikita katika mafunzo ya muda mrefu na mfupi pamoja na kuleta madaktari bingwa kutoka China kutoa huduma katika hospitali za kibingwa hapa nchini.

Akizungumza leo Januari 25, 2022 katika hafla ya kupokea madaktari bingwa hao Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dk Respicious Boniface amesema ujio wa madaktari bingwa hao ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuboresha huduma za kibingwa ambapo pamoja na kutoa huduma kwa wagonjwa madaktari hao watafundisha wanafunzi.

“Ujio wa wataalamu hawa una tija kubwa kwa taasisi yetu na kwa nchi kwa ujumla kwani watafanya upasuaji kwa kushirikiana na madaktari bingwa wazalendo jambo ambalo litapelekea kubadilishana uzoefu na kupeana mbinu za kisasa, pia watatoa mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi kwani moja ya malengo ya MOI ni kutoa mafunzo,” Amesema Dk Boniface.

Advertisement Kiongozi wa timu ya madaktari bingwa kutoka China, Dk Meng Yong amasema ni heshima kubwa kupata fursa ya kufanya kazi Tanzania na kuwahudumia watanzania kwa kipindi cha miaka miwili ambapo pia watapata nafasi ya kubadilishana uzoefu na madaktari bingwa wenzao wa Tanzania na kujifunza mambo mengi.

Mwakilishi wa Wizara ya Afya, Dk Vumilia Liggyle amesema ushirikiano baina ya Serikali hizo mbili ni wa kihistoria kwani una zaidi ya miaka 50 na umekuwa ukienziwa kizazi hadi kizazi jambo ambalo limekuwa likiwanufaisha wataalamu kwenda nchini China kupata mafunzo na madaktari bingwa kutoka China kuja nchini kutoa huduma.

“Tumepokea madaktari bingwa 11 kutoka China, watatoa huduma za kibingwa katika maeneo mbalimbali hapa nchini kwa miaka miwili katika hospitali zetu za kibingwa za MOI, JKCI, MNH na hospitali ya kanda ya rufaa Mbeya (MZRH), amesema Dk Liggyle.

Chanzo: www.mwananchi.co.tz