Dar es Salaam. Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Elisha Osati amesema changamoto kubwa inayowakabili madaktari ni tabia ya baadhi ya viongozi na wanasiasa kuagiza wataalam wa afya wanaofanya kosa la kitaalam kuwekwa ndani.
Dk Osati amesema hayo leo Alhamisi Februari 20, 2020 katika mkutano wa madaktari na watumishi wa sekta ya afya unaofanyika katika ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.
Amesema sheria inayowapa mamlaka viongozi wa Wilaya na Mikoa kuwaweka watu ndani masaa 48 imekuwa mwiba kwa taaluma ya utabibu.
“Kumekuwa na tabia ya viongozi wa kisiasa kwenda hospitali na kukuta kosa limefanyika, anapokuja kiongozi mkuu wa wilaya, mkoa na viongozi wengine wa kisiasa akisema weka ndani daktari, mfamasia au nesi hatudhni kuwa inatutendea sawa” amesema.
Amesema katika changamoto wanazozipata katika kazi zao hiyo ni kubwa.
“Katika changamoto tunayoipata kwenye taaluma, hii ni kubwa kwa sababu inatuondolea heshima ya taaluma,” amesema.
Pia Soma
- Uchunguzi wa miaka 34 mauaji ya waziri mkuu kukamilika Juni
- Iran yagoma kukabidhi kisanduku cheusi cha ndege ya Ukraine
- Moi kuanza upasuaji wa ubongo Machi 2020
“Tuna sheria zetu zinazoshughulikia kosa la kitaaluma, lakini sasa hii ya kumuweka mtu ndani tunaona haitutendei haki” amesema rais huyo wa MAT na kuongeza.”
“Ile sheria ya kuweka watu ndani masaa 48 kwa kweli imekuwa mwiba mchungu sana kwenye taaluma zetu, tunaomba utoe maelekezo kwa viongozi hawa waache hii tabia na wafuate sheria na taratibu za kitaaluma zilizoko,” amesema rais huyo huku akipigiwa makofi mara kwa mara na madaktari waliohudhuria mkutano huo.
Mkutano huo unaoendelea umehudhuriwa na Rais John Magufuli; naibu Waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile; Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla na viongozi wengine wa Serikali.