Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Madaktari Bingwa kupiga kambi matibabu Musoma

Picha Saratani Data Madaktari Bingwa kupiga kambi matibabu Musoma

Mon, 12 Jun 2023 Chanzo: Mwananchi

Jumla ya watu 45 kati ya 1, 302 waliofanya vipimo vya saratani katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Mara mwaka jana walibainika kuwa na saratani ya shingo ya kizazi.

Akizungumza mjini Musoma leo Juni 12, 2023 wakati wa hafla ya kuzindua wiki ya huduma za kibingwa kwa kwa wagonjwa wa Saratani, Daktari Bingwa wa magonjwa ya akinamama kutoka Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Mara, Dk Patrick Kenguru amesema mkoa huo ni miongoni mwa mikoa nchini yenye idadi kubwa ya wagonjwa wa saratani.

"Tunaishukuru Serikali kwa ujio wa Madaktari Bingwa watakaotoa huduma kwa wakazi wa Mkoa wa Mara katika kambi hii ya wiki moja; natoa wito kwa wananchi kujitokeza kufanyiwa vipimo, kupata ushauri na tiba kwa watakaobainika kuwa na saratani,’’ amesema Dk Kenguru

Ametaja baadhi huduma zitakazotolewa kwa wananchi bila malipo kuwa ni uchunguzi na matibabu ya saratani ya shingo ya kizazi, matiti na tezi dume.

Pamoja na kuanzishiwa huduma za awali, Dk Kenguru amesema watu watakaobainika kuwa na ugonjwa wa saratani watapewa huduma na tiba ya awali kabla ya kupewa rufaa kwenda Hosptali ya Rufaa ya Kanda Bugando jijini Mwanza kwa matibabu zaidi.

Meneja Kitengo cha Uchunguzi na Dawati la Elimu kwa Umma wa Taasisi ya Saratani Ocean Road, Dk Maguha Stephano amesema jumla ya Madaktari Bingwa 15 wa ugonjwa wa saratani watahudumia wakazi wa Mkoa wa Mara katika kambi hiyo ya wiki moja.

‘Zaidi ya watu 1, 000 wanatarajiwa kupatiwa huduma ya uchunguzi, ushauri na tiba katika kipindi hicho,’’ amesema Dk Maguha

Akizungumzia hali ya saratani nchini, Dk Maguha amesema zaidi ya asilimia 75 ya wagonjwa wanaopokelewa Ocean Road wanakuwa katika hatua ya juu ya ugonjwa, hali inayosababisha matibabu yao kuwa magumu.

‘’Ugonjwa wa saratani unatibika na kupona iwapo atagundulika katika hatua za awali; nawasihi Watanzania wajenge utamaduni wa kuchunguza afya zao mara kwa mara,’’ ameshauri mtaalam huyo

Juma Moshi, mmoja wa wakazi wa Manispaa ya Musoma ameishukuru Serikali kwa kutekeleza utaratibu wa kambi za matibabu ya kibingwa katika maeneo ya pembezoni ambako kuna uhaba wa madaktari na vifaa tiba vya kibingwa.

Chanzo: Mwananchi