Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maambukizi ya VVU yapungua Arusha

Wed, 29 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Arusha. Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi wamefanikiwa kushusha kiwango cha maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) mkoani hapa kutoka asilimia 3.2 mwaka 2011/2012 hadi kufikia asilimia 1.9 katika kipindi cha mwaka 2017/2018.

Mganga mkuu wa mkoa wa Arusha, Dk Timothy Wonanji alisema hayo wakati akitoa salamu za mkuu wa mkoa huo, Mrisho Gambo wakati wa uzinduzi wa kampeni ya Furaha Yangu inayolenga kuwahamasisha wananchi kupima VVU na kuanza kutumia dawa za ARV.

Alisema matokeo hayo mazuri ni mwendelezo wa mapambano dhidi ya ugonjwa hatari wa Ukimwi katika kipindi cha miaka 30 na kila mmoja anatakiwa kutimiza wajibu wake kuutokomeza kabisa.

"Changamoto kubwa ipo kwa wanaume kujitokeza kupima virusi vya Ukimwi, takwimu za mwaka 2016/2017 zinaonyesha watu wenye umri wa miaka 15 hadi 64 waliopima kujua hali zao wanawake walikua asilimia 54.7 wakati wanaume walikua asilimia  45.3,"alisema Dk Wonanji.

Alisema hadi kufikia Desemba 2017 mkoa umefanikiwa kupima VVU watu 188,159 ambalo ni ongezeko la watu 53,223 ikilinganishwa na watu waliopima mwaka 2016 ambao ni 134,936.

Kwa upande wake Meneja Mradi Msaidizi wa shirika la Elizabeth Glaser Pediatric AIDS Foundation (EGPAF) mkoa wa Arusha, Jonathan Yona alisema kupitia mradi wa USAID Boresha Afya wanashirikiana na serikali katika mapambano ya Ukimwi, Kifua Kikuu(TB), Uzazi wa mpango na ukatili wa kijinsia.

Alisema huduma hizo zinapatikana kwenye vituo 59 vilivyopewa kipaumbele kwanye halmashauri zote saba za mkoa wa Arusha na kuwa kampeni ya Furaha Yangu itasaidia kuongeza hamasa ya wananchi kujitokeza kupima na wanaogundulika wameambukizwa kuanza dawa mara moja.

Naye ofisa programu wa taasisi ya Benjamini Mkapa Foundation mkoa wa Arusha, David Mnkhally alisema katika kushirikiana na serikali kuimarisha huduma za afya ikiwemo Ukimwi watatekeleza mradi wa miaka mitatu wenye kufanya upimaji jumuishi wa maambukizi ya virusi vya Ukimwi.

Alisema upimaji jumuishi ulioanza Agosti 17 mwaka huu katika kata ya Monduli Juu watu waliopima ni 2,987 kati yao 1,781 sawa na asilimia 59.6 ni wanaume na 1,206 sawa na asilimia 40.4 ni wanawake na kati yao tisa wamekutwa na maambukizi.

Chanzo: mwananchi.co.tz