Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maambukizi ya VVU Mara yaongezeka, sababu zatajwa

Ukimwi Mwanafunzi Maambukizi ya VVU Mara yaongezeka, sababu zatajwa

Tue, 12 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kiwango cha maambukizi ya Ukimwi mkoani Mara kimeongezeka kutoka asilimia 3.6 miaka mitano iliyopita hadi kufika asilimia 5 mwaka jana.

Hali hiyo inatokana na sababu mbalimbali zikiwemo za kiuchumi na kijamii huku jamii ikitakiwa kushiriki moja kwa moja katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo.

Takwimu hizo zimetolewa leo, Desemba 12, 2023 na Mratibu wa Upimaji Ukimwi na Tohara Kinga Mkoa wa Mara, Felix Mtaki kwenye mafunzo ya waandishi wa habari yaliyoenda sambamba na utambulisho wa mradi wa Afya Thabiti.

"Hali ni mbaya kuna kila sababu ya kila mmoja kushiriki katika mapambano haya, kiwango hiki ni kikubwa kuliko hata kiwango cha Taifa ambacho ni asilimia 4.5," amesema

Ametaja baadhi ya sababu zinazosababisha ongezeko hilo ni uwepo wa shughuli za uchimbaji madini, uvuvi, mila na tamaduni.

"Mfano kuna baadhi ya jamii hazifanyi tohara kwa wanaume na kitaalamu tohara inasaidia kuepuka maambukizi ya Ukimwi kwa asilimia 60, sasa kama jamii haifanyi tohara kwa wanaume unaweza kuona jinsi kulivyo na hatari ya kupata maambukizi mapya kwenye jamii hiyo," amefafanua.

Amesema uwepo wa mtandao wa wanaofanya biashara ya ngono ni sababu nyingine iliyochangia ongezeko hilo na jamii ina jukumu kubwa la kufanya kwenye mapambano hayo badala ya kuiachia Serikali na wadau.

"Utafiti umeonyesha kwa ‘Dadapoa’ 26 kati ya 100 wana Ukimwi na kama mnavyojua mkoa wa Mara kuna shughuli kubwa za uchimbaji wa madini na uvuvi na mambo mengine kwa hiyo kuna uhusiano mkubwa wa kundi hili la Dadapoa na shughuli hizo za kiuchumi," amefafanua.

Baadhi ya waandishi wa habari mkoani Mara wakiwa kwenye mafunzo maalum yaliyoandaliwa na mradi wa Afya Thabiti unaotekelezwa na shirika la Amref mmoani humo.

Akifungua mafunzo hayo ya siku tatu, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara, Dk Zabron Masatu amesema ushirikiano wa waandishi wa habari unahitajika kwa kiasi kikubwa ili kuwezesha mapambano hayo kufikia malengo.

"Dunia inalenga kuwa ifikapo mwaka 2030 kusiwepo na maambukizi ya Ukimwi na hili litafanikiwa endapo waandishi pia watashiriki kikamlifu kwa sababu hata tukipanga mikakati na waandishi wasifikishe ujumbe kwa jamii, itakuwa kazi ngumu kuyafikia malengo," amesema.

Mratibu wa Kudhibiti Ukimwi Mkoa wa Mara, Dk Omari Gamuya amesema ipo mikakati kadhaa inayotekelezwa mkoani humo ili kuhakikisha kasi ya maambukizi mapya inapungua.

Amesema huduma bora kwa wagonjwa wa Ukimwi ni moja ya mikakati hiyo ambapo amesema Serikali hivi sasa imeboresha huduma hasa za tiba kwa wagonjwa hali ambayo inachangia kwa kiwango kikubwa kupunguza maambukizi mapya.

"Kuna utoaji wa huduma za dawa na tiba kwa wagonjwa kwa kutumia alama za vidole, hii imesaidia katika kuwatambua na kuwapa huduma wahusika sahihi lakini pia kuna kampeni mbalimbali zinafanyika kwa ajili ya kutoa elimu kwa jamii kuwajengea uelewa juu ya madhara ya ugonjwa na namna ya kujikinga," amesema.

Amesema mradi wa Afya Thabiti unaotarajiwa kutekelezwa kwa muda wa miaka mitano mkoani Mara chini ya Amref ni moja ya mikakati ya kupambana na ugonjwa huo na kwamba mradi huo utahusisha masuala ya kinga na huduma za tiba.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live