Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maambukizi, vifo vya Covid-19 sasa vyaelemea wasiochanjwa

Walipimapic Data Maambukizi, vifo vya Covid-19 sasa vyaelemea wasiochanjwa

Tue, 8 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati serikali ikiendelea na kampeni ya kuchanja bure wananchi kuwakinga na Ugonjwa wa Virusi vya Corona (Covid-19), idadi ya maambukizi na vifo imezidi kuelemea kwa watu ambao hawajapata chanjo.

Taarifa ya mwenendo wa ugonjwa huo kwa kipindi cha kuanzia Februari 5 hadi Machi 4, inaonyesha asilimia 94.1 ya watu waliopata maambukizi ya ugonjwa huo nchini, ni ambao hawakuchanjwa, wakati vifo vyote nane katika kipindi hicho vilitokea kwa wagonjwa ambao hawakupata chanjo.

Taarifa hiyo ya Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Alfello Sichalwe ya Machi 7, imekuja wakati kasi ya uchanjaji nchini ikisuasua licha ya serikali kutoa huduma hiyo bure kuanzia Julai 28, 2021.

Mbali ya kutofikia chanjo, baadhi ya watu wamekuwa wakisita kufuata kinga hiyo kutokana na imani za kidini, hofu ya athari zake na wengine kusubiri kuona ufanisi wake.

Mlipuko wa wagonjwa wa Covid-19, ambao hushambulia mfumo wa kupumua, uliibukia China Desemba, 2019 na kusambaa kwa kasi duniani, huku Tanzania ikithibitisha mgonjwa wa kwanza Machi, 2020. Hadi sasa Covid-19 imeua karibu watu milioni sita kote duniani, kwa mujibu wa takwimu zilizokusanywa na shirika la habari la AFP.

Marekani ndiyo inaongoza kwa kurekodi vifo vingi baada ya watu wake 958,621 kupoteza maisha, ikifuatiwa na Brazil (652,143) na India (515,102).

Taarifa hiyo ya Mganga Mkuu wa Serikali iliyotolewa jana inasema tangu kuingia kwa ugonjwa huo Machi, 2020, watu 800 wameshapoteza maisha, ikiwa ni asilimia 2.4 ya watu 33,726  waliothibitika kuwa na maambukizi baada ya watu 471,965 kupimwa.

"Kwa hapa nchini katika kipindi cha tarehe 05 Februari hadi 04 Machi 2022, visa vipya 290 vya waliothibitika kuwa na maambukizi viliripotiwa kati ya watu 31,090 waliopimwa (sawa na asilimia 1)," inasema taarifa hiyo ya Mganga Mkuu wa Serikali.

Kuhusu wasiochanjwa, taarifa hiyo inasema "katika kipindi cha tarehe 5 Februari na tarehe 4 Machi 2022, wagonjwa wapya 136 walilazwa, kati yao 128 (sawa na asilimia 94.1) walikuwa hawajachanjwa.

"Kwa siku ya tarehe 04 Machi, wagonjwa mahututi wanne waliripotiwa na wote walikuwa hawajachanjwa. Vifo nane (8) vimeripotiwa katika kipindi cha tarehe 05 Februari hadi 04 Machi 2022 kutoka mikoa ya Mwanza (wamefariki watu watano), Dodoma (2), Kagera (1) na wote walikuwa hawajachanjwa."

Rais Samia Suluhu Hassan alizindua kampeni ya kuchanja Julai 28 mwaka jana, akiwasihi wananchi kujitokeza kupata kinga hiyo ili kujinga na ugonjwa huo.

Rais Samia amekuwa akisisitiza kuwa kuchanja ni hiari, lakini amekuwa akieleza athari za kutochanja dhidi ya ugonjwa huo uliozorotesha shughuli za kiuchumi, kijamii na kiutamaduni duniani baada ya kulipuka mwaka 2019.

Tanzania ililazimika kufunga shule na vyuo mwaka 2020 baada ya kuwepo na ongezeko la maambukizi, lakini ilisitisha kutoa taarifa za maendeleo ya ugonjwa huo miezi michache baadaye kutokana na serikali kuwa na wasiwasi na vifaa vya vipimo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live