HALMASHAURI ya Wilaya ya Nyang’hwale mkoani Geita imefanikiwa kupunguza kiwango cha maambukizi ya ugonjwa wa Malaria kwa asilimia 4 kutoka asilimia 20.1 mwaka 2018 hadi asilimia 16.1 kwa mwaka 2022.
Mratibu wa Kampeni ya Kudhibiti Malaria Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale, George Ndukwa amebainisha hayo wakati akisoma taarifa ya mapambano dhidi ya ugonjwa huo kwa kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa mwaka 2023.
Amesema, hatua hiyo ni matokeo ya utoaji elimu ya afya, kugawa vyandarua bure kwa wajawazito na watoto chini ya miaka mitano, utoaji wa dawa kinga za malaria kwa wajawazito na unyunyiziaji dawa ya kuua vimelea vya malaria.
Ameeleza, kwa mwaka 2021 hadi 2023 jumla ya vyandarua 21,727 viligawiwa kwa wajawazito, vyandarua 23,747 viligawiwa kwa watoto wa miezi tisa na vyandarua 63,417 viligawiwa kwa wanafunzi wa shule 74 za msingi.
“Jumla ya lita 107 zitatumika kuangamiza kiluwiluwi kwenye mazalia ya mbu yaliyopo kata ya Nyijundu, Kharumwa, Kakora. Kiua dudu kimeagizwa kwa bajeti ya 2022/23 kutoka kiwandani kina thamani ya Shilingi milioni 1.4.”
Awali Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigela amesema kiwango cha maambukizi ya ugonjwa wa Malaria mkoani humo ni asilimia 13 kwa mjibu wa utafiti wa Tanzania Demographic Health Survey (TDHS) mwaka 2022.
Aidha Shigela amebainisha kuwa mkoa umeweza kupunguza idadi ya wagonjwa waliogundulika kuwa na Malaria kwa asilimia 11 kutoka wagonjwa 261,062 mwaka 2021 hadi wagonjwa 232,821 kwa mwaka 2022.
Ameeleza katika kuendeleza mapambano dhidi ya malaria mkoani Geita, mwaka 2022 pekee, jumla ya vyandarua 23,398 viligawiwa kliniki ya wajawazito na watoto chini ya miaka mitano ikiwa wajawazito ni 12,286 na watoto 11,112.
Amesema pia mkoa umeimarisha upimaji wa wagonjwa wenye homa kwa asilimia 73 na kuhakikisha upatikanaji wa dawa za Malaria na vitendanishi vya kipimo cha mRDT kwa zaidi ya asilimia 90% kwenye vituo vya huduma za Afya.
Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa mwaka 2023, Abdala Shaibu Kaimu ameagiza watalaamu wa afya kuongeza nguvu ili kufikia adhima ya kutokomeza malaria kitaifa na kupunguza vifo vya wajawazito na watoto.