Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maajabu ya mkojo wa binadamu

53247 Pic+mkojo

Sat, 20 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kinachotoka kwenye kibofu chako cha mkojo kinaweza kuwa faida shambani, kwani mkojo unaweza kuwa mbolea nzuri kwa hiyo hakuna haja ya kuumwaga kama taka.

Mkojo wa binadamu unasemekana kuwa na virutubisho muhimu vinavyofanya kazi haraka kama naitrojeni, fosforasi, potasiamu na virutubisho vingine vinavyohitajiwa na mimea kwa mujibu wa mgunduzi wa mbolea hiyo, Laulian Mchau.

“Mkojo wa binadamu ni msafi na hauna vijidudu kama bacteria. Yaani ni msafi kiasi kwamba unaweza kuunywa kama ndiyo kwanza unatoka. Lakini ukiachwa kwa zaidi ya saa 24 unabadilika na kuwa ammonia inayokuwa na harufu,” anasema Mchau.

Katika hali hiyo anasema unakuwa mkali kwa matumizi ya mimea.

Maelezo yake kwa gazeti dada la Mwananchi la The Citizen yanaonyesha kuwa, kama wakulima na wenye bustani wakiuchanganya mkojo na sehemu 10-15 ya maji unaweza kutumika kukuzia mimea yao.

Vilevile, kuchanganya sehemu 30-50 ya maji na mkojo unaweza kutumika kwenye mimea inayopandwa kwenye chungu inayopendelea mbolea ya aina hiyo.

Mbolea ya mkojo ni nzuri na inafaa kutumika moja kwa moja kwenye mizizi ya mimea.

Kuna virutubisho muhimu vinavyopatikana katika mkojo ikiwamo naitrojeni, urea, tindikali ya uric, ammonia, potasiamu, kalisiamu, mangenisiam, sodiam, kloraidi, salfeti na fosfeti.

Wakati wa kukojoa, Mchau anasema mtu mzima hutoa gramu 11 za naitrojeni na urea, gramu moja ya fosforasi/super-phosphate na gramu 2.5 ya potasiamu.

“Ukitumia mkojo kukuza mimea mara moja kwa wiki kwa angalau miezi miwili utaongeza mazao mara dufu,” anasema Mchau.

Ukusanyaji wa mkojo

Mchau anataja maeneo ya kukusanyia mkojo kuwa ni pamoja na vyoo vya umma na vyoo vinavyotembea.

Mpaka sasa amekuwa akikusanya wastani wa lita kati ya 25 hadi 40 kwa siku kutoka kwa wanafamilia wenzake na vyoo vya shule.

“Nawalipa Sh1,000 kwa lita ya mkojo. Hawakojoi tena porini, pembeni ya miti au kwenye bustani za maua lakini kwenye vyombo maalum tu. Wanatenganisha mkojo na taka nyingine ili kuufanya kuwa msafi, wakikojoa kwenye chupa au ndoo au vyoo maalum vilivyotengwa,” anasema.

Anasema kwa wastani mtu mmoja hukojoa mara tano kwa siku na kupata lita 2.5.

Kama hiyo haitoshi, Mchau ana mpango wa kununua mkojo kutoka kwenye vyoo vya umma na vyoo vinavyotembea akilipa Sh500 kwa lita, huku pia akipanga kuwahusisha wahandisi wa majengo kujenga vyoo vitakavyokuwa na njia ya kukusanya na matangi ya kuhifadhia mkojo.

Anasema vyoo vingi hukusanya kati ya lita 50 hadi 100 za maji kusafishia lita 1.5 ya mkojo kwa siku.

Njia ya kutengeneza

Mchau anayo mashine maalum ambayo huitumia kuchakata mkojo uliokusanywa kwa kuondoa gesi na kuongeza virutubisho vinginevyo ili kuifanya kuwa mbolea.

Mashine hiyo aliitengeneza mwenyewe miaka 15 iliyopita kwa gharama ya Sh4 milioni.

Uwezo wake ni kuchakata na kutengeneza angalau lita 500 kwa mwezi, lakini kwa sasa anachakata lita 300 kutokana na upungufu wa vifaa. “Lita moja ya mkojo inaweza kuzalisha hadi lita 2.5 za mbolea. Pia lita 10 za mkojo zinaweza kutumika kwenye ekari moja ya mazao,” anasema.

Anasema lita moja ya mbolea ya mkojo inauzwa Sh3,500 kwa kwa ajili ya kuchanganya na maji na Sh7,000 kwa mbole isiyochanganywa.

Umuhimu wa mbolea ya mkojo

Matumizi ya mkojo badala ya kuumwaga kuna kupunguza uchafuzi wa maji. Mkojo ni chanzo muhimu cha naitrojeni ambayo kama haitatolewa kwenye maji husababisha malimbikizo ya kemikali kwenye maji zinazokwamisha ukuaji wa mimea.



Chanzo: mwananchi.co.tz