Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

‘Maabara ya Taifa haitapokea wasafiri kuhusu sampuli za corona’

2e7b94e98f30c2829eafbec16263d3df ‘Maabara ya Taifa haitapokea wasafiri kuhusu sampuli za corona’

Mon, 1 Mar 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeiondoa maabara ya taifa katika chaguo la kituo cha kutolea sampuli za kupima ugonjwa wa homa kali ya mapafu (Covid -19) kwa wasafiri katika mfumo wa kutuma miadi.

Taarifa hiyo ilitolewa jana katika vyombo vya habari ikisainiwa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali wa Wizara hiyo ,Gerard Chami, ilisema Maabara ya Taifa ya Afya imekuwa na changamoto ya wasafiri wanaofika kwa wingi na kusababisha msongamano hali inayosababisha huduma za maliwato na maeneo ya kuegesha magari kuwa finyu.

“Kuanzia Machi 1, 2021 Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii haitapokea wasafiri ili kuwachukua sampuli badala yake itabaki na jukumu la kupima na kutoa vyeti ambalo ndilo jukumu lake la msingi,” ilisema taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, utaratibu wa kupima sampuli kwa kipimo cha haraka cha protini za kinga, utaendelea kufanywa na maabara hiyo kwa utaratibu uliokuwepo wa kufika katika maabara ya taifa kuchukuliwa sampuli na kupata cheti cha kipimo kwa wasafiri wanaohitaji kipimo hicho kutokana na matakwa ya nchi wanakoenda.

Ilisema wasafiri wanaohitaji kipimo cha haraka cha Covid -19 cha Antigen wataendelea kupimwa katika Kiwanja cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) na Kilimanjaro (KIA) yakiwa ni matakwa ya ndege zao ambapo watapimwa saa nne kabla ya ndege kuondoka.

Taarifa hiyo iliwataka wasafiri wote kwenda katika vituo vya kuchukulia sampuli kama ilivyotolewa kwenye Mwongozo wa Ushauri kwa Wasafiri.

Chanzo: habarileo.co.tz