Katika kuiunga mkono Serikali katika sekta ya afya, Kanisa la Kilimanjaro International Christian Centre (KICC) lililopo mkoani Kilimanjaro kwa kushirikiana na wadau kutoka nchini Marekani wameanza mchakato wa kujenga maabara ya kisasa ya uchunguzi wa magonjwa, yakiwamo saratani.
Maabara hiyo itakuwa ya kwanza kupatikana katika nchi za Afrika Mashariki na kati na itatoa huduma nyingine mbalimbali za kiuchunguzi wa magonjwa mbalimbali ya binadamu.
Maabara hiyo ambayo ujenzi wake unatarajiwa kuanza mwaka 2022 itagharimu dola za kimarekani milioni 30 ambapo itasaidia kuwapunguzia adha wananchi ambao wamekuwa wakifuata matibabu nje ya nchi na kutumia fedha nyingi kwa ajili ya matibabu.
Akizungumza na Gazeti hili leo, Oktoba 22 ofisini kwake, Askofu Mstaafu wa kanisa la Assemblies of God (TAG) na mchungaji kiongozi wa kanisa la KICC, Askofu Glorious Shoo amesema katika mambo ambayo yamekuwa yakiwatesa watu wengi ni umbali wa kupata huduma stahiki kama ambavyo Mataifa mengine yanapata kirahisi.
"Kanisa letu limejikita katika kutamani kuleta mabadiliko kupata mahali ambapo watu wanaweza kuja na kupima magonjwa mbalimbali na kuweza kupata suluhisho la haraka,hivyo tumedhamiria kuanzisha mradi mkubwa wa kujenga jengo la maabara ya kisasa ambalo litagharimu dola za kimarekani milioni 30.
Amesema kuwa maabara hiyo itakuwa miongoni mwa maabara kubwa katika ukanda huu wa Afrika Mashariki.
“Hivyo itasaidia kupunguza changamoto ambayo imekuwa ikiwafanya wagonjwa kukimbilia matibabu nje ya nchi na kutumia fedha nyingi kwa ajili ya matibabu," amesema Askofu Shoo.