Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MSD yaongeza uzalishaji barakoa kwa siku

59dbf31cabfabb20e26b9148113b31ec.png MSD yaongeza uzalishaji barakoa kwa siku

Tue, 23 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

BOHARI ya Dawa (MSD) imeongeza wateja wa barakoa inazozalisha kutoka vituo vya afya hadi kwa wananchi, taasisi na mashirika hivyo kuongeza mahitaji.

Bohari hiyo ilianza uzalishaji wa barakoa hizo tangu Agosti mwaka jana ambapo kwa saa inazalisha barakoa 4,800 na kwa siku wastani wa barakoa 40,000.

Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Meja Jenerali Gabriel Mhidze, alisema jana kuwa kutokana na ongezeko la mahitaji bohari hiyo inatarajia kuongeza uzalishaji wa barakoa.

Alilieleza HabariLEO kuwa barakoa zao zinatengenezwa kwa malighafi zenye ubora wa kimataifa hivyo zina ufanisi wa kuchuja vimelea ya zaidi ya asilimia 95 hivyo kumwezesha mtumiaji kwa salama zaidi na apumue vizuri bila shida.

Aidha, alisema barakoa hizo zina alama ya MSD na zinauzwa kwa Sh 600 kila moja, barakoa tano Sh 3,000 na barakoa 10 Sh 6,000.

“Mahitaji hapo awali yalikuwa ya kawaida, kwani tulikuwa tunaviuzia vituo vya afya ambao ndio wateja wetu, ila kwa sasa mahitaji yameongezeka,” alisema Meja Jenerali Mhidze.

Alisema barakoa za MSD sasa pia zinapatikana kwenye kanda 10 ambazo ni Tanga, Kilimanjaro, Mwanza, Dar es Salaam, Tabora, Mtwara, Dodoma, Kagera, Mbeya na Iringa.

Meja Jenerali Mhidze alisema pia zinapatikana kwenye maduka ya MSD yaliyopo Hospitali ya Mount Meru Arusha, Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), nje ya Hospitali ya Rufaa Mbeya, nje ya hospitali ya Rufaa ya Sekou Toure Mwanza, Hospital ya Wilaya Chato, Hospital ya Wilaya Ruangwa mkoani Lindi na Katavi.

Pamoja na barakoa hizo za MSD, biashara ya bidhaa hiyo imeshamiri mitaani na kwenye maduka ya dawa.

Katika maeneo mengi Dar es Salaam barakoa zinazotengenezwa mitaani zinauzwa Sh 500 hadi 1,000 kulingana na ubora wake na kwenye maduka ya dawa ni Sh 2,000 kwa barakoa moja.

Chanzo: habarileo.co.tz