Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MSD waadhimisha siku ya wanawake wodini

MSD waadhimisha siku ya wanawake wodini

Sun, 10 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wafanyakazi wanawake kutoka Bohari Kuu ya Dawa Tanzania (MSD) wameadhimisha siku ya mwanamke duniani kwa kutoa zawadi mbalimbali katika wodi ya watoto waliozaliwa kabla ya wakati (njiti) ya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

Zawadi hizo ni pempasi, kanga, sabuni za kufulia na kuogea, mafuta ya kupaka na dawa za meno vyenye thamani ya Sh2.8 milioni ambazo zimetolewa leo Ijumaa Machi 8, 2019.

Alizungumza wakati wa kukabidhi zawadi hizo mwenyekiti  wa wafanyakazi wanawake MSD, Rehema Mosha amesema wamechagua siku hiyo muhimu ambayo huadhimishwa Machi 8 kila mwaka duniani kote, kuwafariji wale ambao wamekosa nafasi ya kujumuika katika majukwaa mbalimbali.

“Zawadi hizi ni ishara ya upendo lakini pia tumeona watoto njiti wana uhitaji mkubwa kwa sababu wanakaa hospitali muda mrefu kwa hiyo tunaamini zawadi hizi ni sehemu ya faraja kwao,” amesema.

Aidha ametoa rai kwa wanawake wote duniani kuacha kubaguana na badala yake wasaidiane katika shida na raha na kuacha tabia ya kudhalilishana.

Daktari  bingwa wa magonjwa ya homoni kitengo cha elimu na utafiti, Dk Faraja Chiwanga ameshukuru kwa msaada huo akiomba taasisi mbalimbali kuwakumbuka watu wenye uhitaji siku zote na siku ya maadhimisho kama ilivyo leo.

“Wodi hii tunaita kangaroo kwa sababu muda wote mtoto anatakiwa kuwa kifuani mwa mama hivyo zawadi hizo kama pempasi vitaondoa usumbufu wa mama kwenda kufua mara kwa mara,” amesema.

“Kuna wakati wanakuwa na uhitaji zaidi kwa sababu wanakaa muda mrefu lakini pia wengine wametoka mbali, hawakujua kama wangepata watoto njiti hivyo hawakujiandaa kimahitaji,” ameongeza.

Ester Muti mmoja wa wazazi katika wodi hiyo na mkazi wa Kisarawe amesema mbali na kusherehekea siku ya mwanamke duniani, amefarijika na ujio wa wanawake kutoka MSD lakini pia kuwakumbuka kwa zawadi.



Chanzo: mwananchi.co.tz